Shabiki aiponza Madrid yatozwa faini

MADRID: SHIRIKISHO la Soka Barani Ulaya (UEFA) limeitoza faini Real Madrid pamoja na kuamuru kufungwa kwa muda sehemu ya viti katika Uwanja wa Santiago Bernabéu baada ya shabiki mmoja kuonekana akifanya ishara inayofanana na saluti ya Nazi.
Shirikisho hilo la soka barani Ulaya limetangaza kuwa Real Madrid italazimika kulipa faini ya euro 15,000 (takribani pauni 13,000 au dola 17,400) kufuatia kile walichokiita “tabia ya kibaguzi ya mashabiki wake.”
Mbali na faini hiyo, klabu hiyo ya LaLiga imeagizwa kufunga viti 500 vilivyopo katika sehemu ya chini ya jukwaa la kusini la Bernabéu kwa mechi moja ya mashindano ya UEFA. Hata hivyo, adhabu hiyo ya kufungwa kwa viti imesimamishwa kwa kipindi cha majaribio cha mwaka mmoja.
Tukio hilo lilitokea kabla ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo Real Madrid iliibuka na ushindi dhidi ya Benfica.
Real Madrid imesema tayari imemtambua shabiki huyo na kumtoa ndani ya uwanja. Katika taarifa yake, klabu hiyo ilisisitiza kulaani vikali vitendo vinavyochochea chuki au vurugu katika michezo na jamii.
“Real Madrid inalaani aina hii ya ishara au kauli zinazochochea vurugu na chuki katika michezo na jamii,” ilieleza sehemu ya taarifa ya klabu hiyo.
Tukio hilo limekuja wiki moja baada ya mshambuliaji wa Real Madrid, Vinícius Júnior kudai kudhalilishwa kwa maneno ya kibaguzi na mchezaji wa Benfica, Gianluca Prestianni. Baada ya uchunguzi wa UEFA, Prestianni alifungiwa mechi moja, adhabu ambayo ilithibitishwa baada ya rufaa ya Benfica kukataliwa.
Hii ni adhabu ya pili ya hivi karibuni kutolewa na UEFA kufuatia madai ya ishara za Nazi katika michezo ya Ligi ya Mabingwa, baada ya Tottenham Hotspur kutozwa faini ya euro 30,000 kufuatia shabiki wao kudaiwa kufanya ishara hiyo katika mchezo dhidi ya Eintracht Frankfurt.




