Serikali yataka mabadiliko watendaji kurugenzi ya michezo

WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa ameelekeza kufanyika kwa mabadiliko ya watendaji kwenye kurugenzi ya michezo ili kupata watu wenye sifa na kiu ya mafanikio, weledi, wachapakazi na wabunifu ili kuleta mabadiliko ya kweli kwenye sekta ya michezo.
Mchengerwa ametoa maelekezo hayo leo, Dodoma katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini, John Mapepele.
Aidha Mchengerwa amemwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kukutana mara moja na Baraza la Michezo la Taifa(BMT) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania(TFF) ili kutathmini mwenendo wa timu ya taifa(Taifa Stars) na kuandaa mkakati wa pamoja wa kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri na kupata mafanikio yanayotarajiwa.
Agizo hilo limetokana na mwenendo usioridhisha wa Taifa Stars ambayo imekuwa ikishiriki mashindano ya kimataifa mara kwa mara bila kufanya vizuri ikilinganishwa na timu nyingine za taifa ikiwemo ya mpira wa miguu kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mchengerwa ameagiza kikao hicho maalum kifanyike mara moja na apokee taarifa ya utekelezaji wa maelekezo hayo ndani ya siku 14 kuanzia leo.
Katika michezo ya hivi karibuni, Taifa Stars ilitolewa na Uganda michuano ya kufuzu kushiriki fainali za ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa ndani(CHAN) kwa jumla ya mabao 4-0 ikichapa nyumbani bao 1-0 na kisha mabao 3-0 nchini Uganda.
Wakati huo huo Waziri Mchengerwa ameielekeza BMT kufuatilia pambano la ngumi la bondia Hassan Mwakinyo lililofanyika Uingereza dhidi ya Liam Smith.
Ieleweke serikali haipo tayari kuona mazingira yoyote ya sintofahamu kwa wachezaji wa kitanzania wanaposhiriki mashindano hasa ya kimataifa.