Samia Netball Cup 2025 yazinduliwa rasmi

DAR ES SALAAM: Mashindano ya mpira wa netball kwa Mkoa wa Dar es Salaam yanayojulikana kama Samia Cup 2025 yamezinduliwa rasmi leo.
Akizungumza na Spoti Leo, Mratibu wa mashindano hayo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Twende Pamoja na Mama Spoti Promotion, Kasimu Ahmad, amesema kuwa lengo la mashindano haya ni kutoa fursa kwa wanawake na mabinti kushiriki katika michezo ya netball huku wakipata nafasi ya kujiimarisha kiafya na kiuchumi.
“Kumekuwa na michezo mingi lakini kwa wakati huu tumeona ni muhimu kuja na mashindano ya netball kwa kuwa wanawake pia wanastahili jukwaa la kuonesha vipaji vyao. Ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia kwa juhudi zake katika kuinua wanawake kupitia michezo,” amesema Kasimu.
Katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza atazawadiwa shilingi milioni 5, kombe na medali. mshindi wa pili atapata shilingi milioni 3 na medali, huku mshindi wa tatu ataondoka na shilingi milioni 1 na laki tano. mshindi wa nne naye atajinyakulia shilingi laki tano.
Mbali na zawadi hizo, mfungaji bora atapewa zawadi ya shilingi laki mbili, na kikundi bora cha hamasa kitapewa zawadi maalum kama njia ya kutambua mchango wao katika kuhamasisha mashabiki na timu.
Kwa upande wake, nahodha wa timu ya Konfoti, Prisca Godlove, aliishukuru serikali kupitia Rais Samia kwa kuandaa mashindano haya yanayowapa wanawake jukwaa la kujiajiri kupitia michezo.
“Tunamshukuru mama Samia kwa kuona thamani ya wanawake katika michezo. Sisi tupo tayari kujiajiri kupitia fursa hizi,” alisema Prisca.
Mchezaji kutoka timu ya Ulipo Tupo, Magreth Elia, alitoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kuutangaza mchezo wa netball ili kuutangaza zaidi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Vyombo vya habari viendelee kutangaza netball ili watoto wa kike wawe na mifano ya kuigwa na wachangamkie michezo hii,” amesema Magreth.