Kwingineko

Ruto ashuhudia mtoto wa Gavana akifunga ndoa ya Kimaasai

NAIROBI: RAIS wa Kenya, William Ruto ameshuhudia harusi ya furaha iliyozungukwa na rangi nyekundu kila kona, wakati mtoto wa Gavana Patrick Ntutu, Jordan Ntutu, alipofunga ndoa na mchumba wake Abigael Moriaso katika hafla ya kuvutia iliyoandaliwa kwa mtindo wa kitamaduni wa Kimaasai.

Hafla hiyo iliashiria muunganiko wa ustaarabu wa kisasa na utamaduni wa jamii hiyo mashuhuri.

Ukumbi wa sherehe ulipambwa kwa rangi nyekundu na nyeupe, huku mapambo ya kitamaduni vito, mikoba ya ngozi na mikeka ya kienyeji iliongeza uhai na umahiri katika sherehe hiyo ya hadhi ya juu.

Wageni walivutiwa na mandhari iliyojawa heshima na utambulisho wa utamaduni wa jamii hiyo.

Bibi harusi Abigael akiwa amevalia gauni jeupe lililong’aa, akipambwa shingoni kwa shanga za Kimaasai ziliongeza uzuri wake huku bwana harusi Jordan akivalia mavazi ya kitamaduni ya Kimaasai yaliyopambwa kwa shanga tofautitofauti, jambo lililofanya wawili hao kuonekana mfano kamili wa mwanga wa tamaduni zao.

Katika tukio hilo la heshima kubwa, Rais William Ruto aliongoza viongozi mbalimbali waliohudhuria. Miongoni mwa wageni mashuhuri walikuwepo ni Waziri wa Afya Aden Duale, Waziri wa Ulinzi Soipan Tuya, Magavana Joseph Ole Lenku wa Kajiado na Lati Lelelit wa Samburu, Seneta wa Narok Ledama Ole Kina, pamoja na wabunge, madiwani na viongozi wengine wengi.

Akitoa hotuba yake, CS Duale aliwasifia maharusi na kusisitiza nguvu ya upendo katika kujenga familia imara. Aliandika pia kwenye ukurasa wake wa X kwamba alifurahia kushuhudia muungano huo, akiwatakia wanandoa maisha yenye amani, furaha isiyoisha, heshima ya pande mbili na uaminifu usiotetereka.

Baada ya kubadilishana viapo, Jordan na Abigael walikata keki ndefu nyeupe iliyopambwa kwa maua halisi, ishara ya mwanzo mpya wenye baraka. Wageni walisherehekea nao kwa furaha huku muziki, nderemo na ukarimu wa Kimaasai ukitawala anga ya sherehe.

Related Articles

Back to top button