Ruediger afanyiwa upasuaji

MADRID:WABABE wa Laliga Real Madrid wametangaza kuwa beki wao machachari Antonio Ruediger amefanyiwa upasuaji wa goti lake la kushoto siku chache baada ya vyomo vya habari nchini Spain kuripoti kuwa Mjerumani huyo mwenye miaka 32 alikuwa anafikiria kufanyiwa upasuaji kutibu tatizo hilo lililomuandama kwa muda mrefu.
Taarifa iliyotochapishwa kwenye website rasmi ya Real Madrid imesema kuwa Ruediger amefanyiwa upasuaji huo leo Jumanne huku ikisema atarejea hivi karibuni baada ya kupona.
“Mchezaji wetu Antonio Ruediger amefanyiwa upasuaji uliofanikiwa kurekebisha mchaniko wa misuli ya chini ya kifuniko cha goti lake la mguu wa kushoto. Ruediger ataanza safari yake ya kupona hivi punde na tunamtakia uponaji wa haraka” – imesema taarifa hiyo.
Ruediger aliwahi kunukuliwa akisema kuwa amekuwa akicheza na na maumivu makali kwenye mguu huo kwa miezi saba. Kupitia mtandao wa X Ruediger ameonesha tamanio lake la kupona haraka na kuwa sehemu ya kikosi cha Kombe la dunia la vilabu na Ligi ya mataifa ya Ulaya.
“Nataka kuwa na uwezo wa kucheza tena haraka iwezekanavyo, kuna michuano miwili mikubwa mbele yangu Nations League na Club World Cup nataka kucheza. Lakini inabidi nijitazame wiki hadi wiki halafu tutaona cha kufanya. Nitafanya kila liwezekanalo niwe sehemu ya michuano hiyo”ameandika Ruediger kwenye X
Ruediger alioneshwa kadi nyekundu kwenye mchezo wa fainali ya Copa del Rey Jumamosi baada ya kuonesha hasira kwa mwamuzi aliyepiga kipyenga kwenye faulo aliyofanya Kylian Mbappe dakika chache baada ya Jules Kounde kufunga bao dakika za mwisho za Extra Time na kuiweka mbele Barcelona, licha ya kuomba radhi Ruediger anakabiliwa na adhabu ya kukosa kati ya mechi nne hadi 12.