Ronaldo ahofia kuzomewa Dublin

DUBLIN: NYOTA wa soka Duniani Cristiano Ronaldo huenda akazomewa na mashabiki wa Ireland katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia utakaopigwa leo Alhamisi, lakini anasema kelele hizo huenda zikasaidia kupunguza presha kwa wachezaji wenzake wa Ureno na kufanya vizuri.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 40, aliyechochea utata huo mwezi uliopita kwa kushangilia kwa kejeli mbele ya beki Jake O’Brien baada ya bao la dakika ya 91 lililofungwa na Ruben Neves katika ushindi wa 1-0, ameahidi kuwa mtulivu zaidi kwenye Uwanja wa Aviva.
Ureno haijapoteza mchezo wowote na inaongoza Kundi F ikiwa na ushindi kwenye michezo mitatu kati ya minne iliyopita, ikihitaji pointi tatu pekee ili kufuzu moja kwa moja kwa Kombe la Dunia la 2026 michuano ambayo Ronaldo anatarajia kushiriki kwa mara ya sita.

“Uwanja utanizomea, lakini nimezoea, Kwa hakika natumai hivyo, labda itawapunguzia wachezaji wengine presha na watafanya vizuri zaidi. Najua itakuwa mechi ngumu sana kwangu, lakini natumai hawatanizomea sana. Nawaahidi nitakuwa kijana mzuri” – amesema Ronaldo
Ireland, ambayo ipo nafasi ya tatu kundi hilo pia, iko pointi sita nyuma ya Ureno na moja nyuma ya Hungary walio katika nafasi ya pili, na inahitaji angalau sare ili kudumisha matumaini ya kucheza ‘playoff’ kabla ya mchezo wao wa mwisho dhidi ya Hungary.
Nahodha wa Ireland Nathan Collins amesema kuwa hakuelewa kwa nini Ronaldo alishangilia vile katika mchezo wa awali mjini Lisbon, akidokeza kuwa huenda kulitokana na kukasirishwa baada ya penalti yake kuokolewa.
Ronaldo, ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Al-Nassr nchini Saudi Arabia, alisema anafurahia kurejea kucheza nchini Ireland licha ya matarajio ya kuzomewa: “,” alisema mshindi wa tuzo tano za Ballon d’Or.
Mshambuliaji huyo ambaye amefunga zaidi ya mabao 950 ya ngazi ya klabu na timu ya taifa, hivi karibuni alidokeza kuwa anakaribia kustaafu soka ndani ya “mwaka mmoja au miwili ijayo.”




