Ribery astaafu soka

WINGA wa zamani wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ufaransa Franck Ribery ametangaza kustaafu mchezo wa mpira wa miguu.
Ribery mwenye umri wa miaka 39 amevunja mkataba wake na klabu ya ligi kuu ya Italia, Salernitana 1919 baada ya kuwa na majeraha ya muda mrefu ya goti.
“Mpira unasimama, hisia hazisimami. Asanteni kila mmoja kwa tukio hili kubwa,” amesema Ribery kupitia mtandao wa Twitter.
Ribery alijiunga na Fiorentina kabla ya kuhamia Salernitana 1919 msimu uliopita akisaidia klabu hiyo kuepuka kushuka daraja kwa pointi moja lakini hajacheza tangu mchezo wa ufunguzi wa Serie A timu yake ilipofungwa na Roma.
Alifunga mabao 124 na kusaidia 182 katika michezo 425 aliyocheza Bayern kutoka 2007 hadi 2019 akishinda Ligi ya mabingwa Ulaya 2013 na mataji 9 ya Bundesliga.