Kwingineko

Raphina masikini anayetikisa Ulaya

TUJIFUNZE kupitia hii ya Raphael Dias Belloli (Raphina), kama ilivyozoeleka kwa wanasoka wengi kutoka Amerika Kusini wametokea kwenye familia duni.

Inaelezwa kuwa kijana huyu alikuwa akitumia kitanda kimoja na wazazi wake pamoja na ndugu zake yaani wanapokezana ili tu kila mtu aionje ladha ya kitanda.

Hivi mnajua kama ‘Birthday’ ya Ronaldinho ndiyo ilibadilisha maisha ya huyu kijana? akiwa na miaka saba alihudhuria birthday ya Gaucho kwasababu kulikuwa na urafiki fulani wa mbali wa mjomba yake kwa Gaucho. Raphina alivyofika pale hakuhangaika na keki alikuwa akilazimisha urafiki na kila aliyemkuta pale na hapo ndipo akaanza kutengeneza urafiki na watu wa mpira.

Njaa ya mafanikio ikamfanya kuwa na ari ya kuvuja jasho lenye thamani ili kuyafikia malengo huku dhamira yake kubwa ikiwa ni kuitafuta heshima ya familia aliyotoka.

Unakumbuka jinsi safari ya Leeds United kwenye EPL ilivyomalizika kwa uchungu msimu mmoja tu tangu walipopanda? kushuka daraja wa Leeds haikuwa story kubwa sana habari ya mjini alikuwa ni Raphina.

Kijana huyu wa Kibrazil mwenye damu ya Italia, alizunguka kwa magoti uwanja mzima akionesha maumivu yake kwa anguko la Leeds, licha ya timu yake kushuka daraja alikuwa ni moja ya wachezaji bora kikosini hapo jambo lililosababisha vigogo mbalimbali Ulaya kuitamani huduma yake.

Klabu ya Barcelona ilishinda vita na kumsajili Julai 2022, wakati anajiunga na Barca alichukuliwa wa kawaida mno na kuna wakati alihusishwa kutolewa kwa mkopo lakini mwanaume huyu mwenye roho ya paka alikomaa na kuonesha uwezo pale anapopata muda wa kucheza.

Kwa sasa Raphina ni moja ya wachezaji viongozi ndani ya Barcelona, jana amefikisha michezo 100 akiwa na timu hiyo. Siku hiyo imekuwa ya kipekee mno kwani alifunga mabao matatu ( hat- trick) kwenye ushindi wa 4-1 Barca wakiinyoa Bayern Munich.

Msimu huu Raphina amehusika kwenye magoli 17 akifunga 9 na kutoa assist 8 kwenye michezo 13 ya msimu huu, chini ya Kocha Hans Flick Raphina amekuwa mwiba mchungu kwa wapinzani. Usikate tamaa mwanangu wewe komaa tu kesho yako inakuja.

Related Articles

Back to top button