Kwingineko

Rammy Galis atunukiwa ubalozi wa bahari Foundation

DAR ES SALAAM: Msanii maarufu wa filamu nchini, Rammy Ahmed Ally, anayefahamika zaidi kwa jina la kisanii Rammy Galis, ametangazwa rasmi kuwa balozi wa Bahari Foundation, taasisi inayojihusisha na utunzaji wa mazingira ya baharini na fukwe za Tanzania.

Akitangazwa mbele ya waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Rammy Galis alieleza kufarijika na kupewa nafasi hiyo ya kipekee na kuahidi kulitumikia jukumu hilo kwa uaminifu, uthubutu, na juhudi.

“Kuwa sauti ya mazingira si jambo dogo kwangu, ni jukumu kubwa nitakalolibeba kwa moyo wote. Tutashirikiana kuhakikisha tunalinda, tunarejesha na kuhamasisha jamii kufanya kwa vitendo,” amesema Rammy.

Ameongeza kuwa, changamoto zinazoikabili bahari ni nyingi, zikiwemo ujazwaji wa taka ngumu kama plastiki, uchafuzi wa maji ya bahari kutokana na majitaka ya majumbani na viwandani, ujenzi holela usiozingatia utunzaji wa mazingira, pamoja na ukosefu wa elimu ya mazingira kwa jamii.

Kwa mujibu wa Rammy, athari za uharibifu wa mazingira ya bahari ni kubwa – ikiwa ni pamoja na kuporomoka kwa utalii wa fukwe, kupungua kwa viumbe wa baharini, kuongezeka kwa magonjwa, kuathirika kwa maisha ya wavuvi na watu wa pwani, pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Bahari si ya kuangalia tu, ni ya kulinda na kutunza. Tunaanzisha kampeni ya usafi wa fukwe, tunatoa elimu kupitia kitabu cha watoto ‘Tilly na Kasa’ kinachofundisha umuhimu wa bahari kuanzia utotoni, na tunahakikisha tunasogeza miundombinu ya kutupa taka kwenye maeneo yenye uhitaji mkubwa,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Faith Yona, Mkurugenzi wa Bahari Yetu, alisema kampeni hiyo itakuwa endelevu na imelenga kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ya bahari kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

“Mnamo Agosti 2, 2025, tutaungana na wanafunzi wa shule mbalimbali katika shughuli za usafi wa fukwe kwa lengo la kuonyesha kwa vitendo dhamira ya kulinda mazingira yetu,” amesema Faith.

Rammy Galis amehitimisha kwa kutoa wito kwa jamii kushiriki kikamilifu kwenye harakati hizi:

“Kama methali isemavyo, moto mingi hujenga mto mkubwa – kila hatua ndogo ni sehemu ya mabadiliko makubwa.”

Related Articles

Back to top button