Rais Samia Ampongeza Simbu kwa Mafanikio Boston Marathon

RAIS Samia Suluhu Hassan, ametoa pongezi kwa mwanariadha wa kimataifa Alphonce Simbu kwa kushika nafasi ya pili katika mbio maarufu za Boston Marathon zilizofanyika nchini Marekani.
“Umefanya kazi nzuri. Ushindi wako ni matokeo ya kujituma kwa bidii, maandalizi mazuri, na nidhamu yako kuanzia jeshini, kwenye mazoezi hadi kwenye mashindano. Umelibeba kwa heshima ya hali ya juu jina la nchi yetu. Endelea kuipeperusha vyema bendera ya Taifa letu,” alisema Rais Samia kupitia ujumbe wake wa pongezi.
Simbu, ambaye ni mwanariadha kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alimaliza mbio hizo kwa muda wa saa 2:05:04, na kuwa wa pili nyuma ya Mkenya John Korir aliyeongoza kwa muda wa saa 2:04:45 — muda wa pili kwa kasi katika historia ya mashindano hayo.
Kwa ushindi huo, Simbu atazawadiwa Dola za Marekani 75,000( sh milioni 201) huku mshindi wa kwanza akipokea Dola 150,000. Mbali na zawadi ya fedha, washindi wa Boston Marathon pia hupokea medali za heshima, mataji au mashada ya maua, na mara nyingi huvutia udhamini mkubwa kutoka kwa makampuni mbalimbali.
Boston Marathon ni moja ya mashindano ya kihistoria na yenye heshima kubwa katika ulimwengu wa riadha, na ushindi wake huambatana na umaarufu wa kimataifa.
Simbu amekuwa miongoni mwa wanariadha wa Tanzania wenye mafanikio makubwa katika historia ya riadha ya kimataifa, na ameendelea kuonesha kiwango cha juu cha ushindani katika jukwaa la dunia.




