PSG wamekutana nacho huko!

PASADENA: Bingwa wa Ligi ya Mabingwa barani ulaya Paris Saint-Germain na mashabiki wao walibaki mdomo wazi baada ya vigogo hao wa soka la Ulaya kuduwazwa na klabu ya Botafogo mabingwa wa Copa Libertadores 2024 bao 1-0 katika mchezo wa Kombe la Dunia la Klabu uliopigwa katika uwanja wa Rose Bowl alfajiri ya leo.
Kabla ya Igor Jesus kufunga bao hilo dakika ya 36 lililokuwa mlima mkubwa kwa PSG kwa dakika zote 90 na za nyongeza, PSG walikuwa hawajapoteza katika mchezo wowote tangu Mei 3 mwaka huu lakini katika mchezo huo mabingwa hao wa Ulaya walionekana kuchoka wakati fulani mbele ya mashabiki 53,699 waliofurika Rose Bowl.
Bao hilo pia lilikuwa bao la kwanza kutikisa nyavu za PSG tangu Mei 17 pale Lassine Sinayoko wa klabu ya Auxerre alipoitangulia mnamo 30 ya mchezo wa Ligue 1. Wafaransa hao walikuwa wamewasunga wapinzani wao watatu wa mwisho kwa jumla ya mabao 12-0 na kushinda Kombe la Ufaransa na fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Staa anayetajwa kuwania Ballon d’Or Ousmane Dembélé ameukosa mchezo wake wa pili mfululizo kutokana na jeraha la misuli ya mbele ya paja yaani ‘quadriceps’ Wenzake bado walitawala mchezo katika kipindi cha kwanza, japo kocha Luis Enrique alifanya ‘rotation’ ya kikosi chake cha kwanza.
PSG walimaliza mchezo huo wakiwa na jumla ya mashuti 16 dhidi ya manne ya Botafogo ambayo yote yalilenga lango huku PSG wakionekana kuwa na safu butu ya ushambuliaji kwani mashuti 16 waliopiga mawili pekee yalimshughulisha golikipa wa Botafogo John Victor.