Kwingineko

Promes sasa kukaa jela nyumbani

AMSTERDAM: Waendesha mashtaka nchini Uholanzi wamesema mchezaji wa zamani wa kimataifa wa taifa hilo Quincy Promes amerejeshwa nchini humo kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu ili kutumikia kifungo jela kwa ulanguzi wa dawa za kulevya na unyanyasaji.

Mahakama ya Uholanzi mwaka jana ilimhukumu mchezaji huyo wa zamani wa Ajax Amsterdam na Spartak Moscow kifungo cha miaka sita bila kuwepo mahakamani kwa kuhusika moja kwa moja na shehena mbili za cocaine kutoka Brazil kupitia bandari ya Antwerp, Ubelgiji, hadi Uholanzi mwaka 2020.

Mwaka 2023, Promes pia alihukumiwa tena kwa mtindo huohuo kifungo cha miezi 18 jela kwa kosa la kushambulia kwa kuhusika na mapigano ya 2020 ambapo alimchoma binamu yake kisu kwenye goti. Promes amekana mashtaka yote na amekata rufaa katika kesi zote mbili.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33, ambaye ana mechi 50 kwa Uholanzi, alikamatwa jijini Dubai mwezi Machi mwaka jana, kwa ombi la waendesha mashtaka wa umma wa Uholanzi alipokuwa kwenye kambi ya mafunzo na Spartak Moscow.

Baadaye aliachiliwa kutoka kizuizini na kuwekwa chini ya vikwazo, ambavyo vilijumuisha kutoruhusiwa kuondoka katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Baadaye Spartak Moscow ilivunja mkataba nae, na akajiunga na klabu ya daraja la pili ya UAE United FC ya Dubai.

Related Articles

Back to top button