Kwingineko

Postecoglou na kismati cha msimu wa pili

BILBAO: KOCHA mkuu wa Tottenham Hotspur, Ange Postecoglou ameendelea kudumisha rekodi yake ya kutwaa kombe kwenye msimu wake wa pili katika kila timu aliyowahi kuifundisha kama kocha mkuu baada ya hapo jana kuiwezesha klabu yake hiyo kutamatisha ukame wa makombe wa miaka 17 baada ya kutwaa ubingwa wa Europa League kwa bao 1-0 mbele ya vigogo Manchester United.

Rekodi hiyo ilianzia katika klabu ya South Melbourne mwaka1996 hadi 2000 alipotwaa kombe la ligi ya taifa ya soka (National Soccer League) akiwa katika msimu wake wa pili katika klabu hiyo ya Australia kabla ya kuhamia Brisbane Roar alikokaa mwaka 2009 hadi 2012 ya nchini humo humo na kushinda taji la A-League Championship katika msimu wake wa pili.

Postecoglou alihama na rekodi hiyo hadi nchini Japan kunako klabu ya Yokohama F. Marinos aliyoitumikia kuanzia msimu wa 2018/19 hadi msimu wa 2020/2021 na msimu wake wa pili yaani 2019/2020 alitwaa ubingwa wa ligi kuu ya Japan (J-League). Awali Postecoglou pia aliitumikia timu ya Taifa ya Australia mwaka 2013–2017 na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa Asia mwaka 2015 na kuipeleka World cup ya 2018.

Rekodi hiyo haikukoma alipotua ulaya kwenye klabu ya Celtic ya Scotland alikodumu tangu mwaka 2021 hadi mwaka 2023. Katika msimu wake wa pili klabuni hapo aliiwezesha Celtic kutwaa ubingwa wa Scottish Premiership na baadae kutimkia kwenye Ligi Kuu ya England kuinoa Tottenham.

Hakuwa na maisha mazuri sana Spurs akimaliza katika nafasi ya sita kwenye ligi akiwa na points 66 baada ya michezo 38 akishinda 20, sare 6 na vipigo 12 nafasi ambayo imemuwezesha kushiriki Europa league katika msimu wake wa pili na kama alivyoahidi ameendeleza rekodi yake kwa kutwaa kombe hilo mbele ya Manchester United ambao msimu ujao wataangalia michuano ya ulaya kwenye Televisheni.

Related Articles

Back to top button