Pogba awaweka Rennes mtegoni

RENNES: KIUNGO wa AS Monaco raia wa Ufaransa Paul Pogba anatarajiwa kurejea uwanjani kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miaka miwili nje ya soka, wakati klabu yake ya Monaco watakapokuwa ugenini dhidi ya Rennes kesho Jumamosi kwenye Ligue 1.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia 2018 amecheza mechi 12 pekee katika misimu mitatu iliyopita kutokana na majeraha, adhabu ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku na sakata la utekaji na ulaghai ambalo yeye ndiye aliyelengwa.
Pogba alipatikana na hatia ya kutumia dawa zilizokatazwa Agosti 2023 akiwa Juventus, na awali alipewa marufuku ya miaka minne, ambayo baadaye ilipunguzwa hadi miezi 18. Hata hivyo, Juventus walivunja mkataba wake Novemba mwaka huohuo, na hivyo kukatisha kwa uchungu kipindi chake cha pili mjini Turin kilichogubikwa na matatizo.

Mwaka 2024, kaka yake Mathias alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani, miwili ikiwa imesitishwa, kwa kuhusika katika jaribio la kumlaghai Pogba kiasi cha euro milioni 13 mwaka 2022.
Ilivyo bahati, Monaco walimpa fursa mpya ya kuokoa kazi lake la soka, wakiamua kumwajiri mara tu alipoanza kupatikana tena baada ya kumalizika kwa adhabu yake Machi mwaka huu. Kiungo huyo mwenye kipaji cha hali ya juu alisaini katika dirisha la majira ya joto, lakini aliwekwa kando ili kufuata mpango maalum wa kumrudisha katika kiwango chake.
Kurejea kwake yamecheleweshwa mara mbili kutokana na majeraha madogo aliyopata msimu huu wa vuli, lakini sasa Pogba aliyewahi kushinda mataji manne ya Serie A na Europa League mwaka 2017 akiwa Manchester United yupo tayari kucheza soka la klabu nchini kwao kwa mara ya kwanza katika maisha yake ya kisoka.
Ingawa sio rahisi kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza Uwanjani Roazhon Park, huenda kocha Sebastien Pocognoli akampa dakika chache za mwisho ili kuanza kumwingiza taratibu katika mfumo wa timu, huku Monaco waliopo nafasi ya sita wakirejea ligi baada ya mapumziko ya kimataifa.

Hata hivyo, macho yote yatakuwa kwa Pogba ili kuona kama uwezo wake wa kupenya kikosini hapo na kujihakikishia nafasi bado upo, kusoma mchezo na kutoa pasi zisizofikika kwa wengi bado upo kama zamani.
Pogba amekuwa akitamani kurejea timu ya taifa ya Ufaransa kuelekea Kombe la Dunia 2026, lakini bado haijulikani kama mwili wake utaweza kuhimili presha za soka la kisasa msimu mzima.
“Kila mchezaji wa Kifaransa hutamani kuiwakilisha Les Bleus, lakini kuna hatua, Hatua ya kwanza ni kurudi na kufanya vizuri. Kuna nafasi za kupigania, na lazima uzitafute.” alisema Pogba aliposaini Monaco.
Katika mechi nyingine za Ligue 1 wikendi hii, vinara Paris Saint-Germain watakutana na Le Havre, Lens waliopo nafasi ya tatu wataikaribisha Strasbourg (nafasi ya nne), huku mahasimu wakubwa wa kusini Nice na Marseille wakitarajiwa kutoa burudani kali.




