Picha za ngono zamponza ‘staa’ wa Benfica

COPENHAGEN: MAHAKAMA nchini Denmark imemkuta na hatia ya kusambaza video ya ngono inayowahusisha wavulana wawili walio chini ya miaka 18 mchezaji wa timu ya taifa ya Norway Andreas Schjelderup, na ikamhukumu kifungo cha nje cha wiki mbili.
Schjelderup, mwenye umri wa miaka 21, ambaye mwaka jana alikuwa akikichezea klabu ya FC Nordsjaelland ya Denmark, aliieleza mahakama ya Copenhagen kuwa alipokea video hiyo ya sekunde 27 kupitia Snapchat na akaisambaza kwenye kundi la Whatsapp marafiki zake wanne.
Winga huyo, anayekipiga kwa sasa katika klabu ya Benfica ya Ureno, alikiri makosa mahakamani na kusema aligundua katika sekunde za mwanzo za video hiyo kuwa watu waliokuwemo hawakuwa na umri wa miaka 18.
“Nilipoipeleka kwa marafiki, nilitambua haraka kuwa ilikuwa kinyume cha sheria, hivyo nikaifuta mara moja,” alisema Schjelderup.

Katika taarifa aliyotoa kupitia Instagram tarehe 8 Novemba, Schjelderup aliomba radhi na kusema alitaka kuwa wazi kuhusu kosa hilo la kijinga alilofanya.
Jaji Mathias Eike alimhukumu kifungo cha nje cha wiki mbili, akimaanisha kuwa ataingia gerezani tu endapo atafanya kosa lingine ndani ya miezi 12 ijayo. Mwendesha mashtaka alikuwa ameomba adhabu ya angalau siku 20 jela.
Mwakilishi wake wa kisheria, Anders Nemeth, aliambia mahakama kuwa upande wa utetezi utachukua muda kufikiria kabla ya kuamua kama watawasilisha ombi la kukata rufaa.
Norway ilifuzu Kombe la Dunia 2026 siku ya Jumapili baada ya ushindi wa 4-1 ugenini dhidi ya Italia, ingawa Schjelderup hakucheza na alibaki kama mchezaji wa akiba katika mchezo huo mjini Milan




