KikapuMichezo Mingine

Pazi, ABC kucheza nusu fainali kikapu

TIMU za mpira wa kikapu za Pazi na ABC zinatarajiwa kukutana nusu fainali ya ligi ya mchezo huo Agosti 28 mkoa wa Dar es Salaam.

Timu hizo zinakutana hatua hiyo baada ya kushinda michezo miwili kila mmoja kati ya mitatu iliyohitajika kwenye hatua ya robo fainali.

Nusu fainali hiyo ya kwanza inatarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Don Bosco Oysterbay.

Pazi imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga Vijana kwa pointi 57-47 mchezo wa kwanza na wa pili 72-41 na kukata tiketi hiyo moja kwa moja.

Kwa upande wa ABC iliifunga Outsiders pointi 69-44 mchezo wa kwanza na wa pili 86-78.

Timu nyingine iliyofuzu hatua hiyo ni Ukonga Kings iliyoshinda michezo miwili dhidi ya Savio kwa pointi 64-63 na 71- 50 hivyo itacheza nusu fainali ya pili dhidi ya JKT au Oilers Agosti 31, mwaka huu.

JKT na Oilers ngoma ilikuwa ngumu baada ya kila mmoja kushinda mchezo mmoja.

Katika mchezo uliopita uliochezwa Jumapili iliyopita, Oilers iliichapa JKT kwa pointi 90-77 lakini katika mchezo wa awali, JKT ilishinda kwa pointi 84-68 hivyo walilazimika kucheza mchezo mwingine mmoja utakaoamua mshindi mmoja wa kucheza na Ukonga Kings.

Mechi ya JKT na Oilers ilitarajiwa kuchezwa jana usiku na pengine tayari mmoja wao amesonga mbele.

Related Articles

Back to top button