Kwingineko

Onana aacha ‘kicheko’ United

MANCHESTER: BAADHI ya mashabiki wa Manchester United wameonekana kufurahia uhamisho wa mkopo wa Kipa wao Andre Onana kwenda klabu ya Trabzonspor ya Uturuki baada ya taarifa rasmi iliyotoka baadaye Alhamisi.

Mashabiki hao wametumia kurasa za mitandao ya kijamii kuelezea furaha yao ya kumuona Onana nje ya milingoti mitatu ya klabu hiyo huku wengine wakiikosoa klabu hiyo kumtoa kwa mkopo usio na kipengele cha kumnunua, wakitaka angeuzwa moja kwa moja.

Dalili za kuondoka kwa Onana zilikuwa dhahiri tangu klabu hiyo ilipomnunua Senne Lammens kutoka Royal Antwerp kwenye siku ya mwisho ya dirisha la usajili jumatatu ya wiki iliyopita.

Usajili wa Lammens wa pauni milioni 18.2 uliifanya United kuwa na makipa wanne, licha ya klabu hiyo kusema haikuwa tatizo kuwa na idadi hiyo ya makipa, mustakabali wa Onana tayari ulikuwa shakani.

Mlinda lango wa kimataifa wa Uturuki Altay Bayindir ameanza katika mechi zote tatu za Ligi msimu huu, wakati Onana mwenye umri wa miaka 29 amecheza moja pekee, mechi ya raundi ya pili ya Kombe la Carabao dhidi ya Grimsby waliyopoteza kwa penalti. Onana akilaumiwa kufanya makosa yaliyozaa mabao mawili ya Grimsby.

Onana alisajiliwa kutoka Inter Milan kwa pauni milioni 47.2 mwaka 2023, panda shuka kwenye kiwango chake imemfanya kukosolewa vikali tangu wakati huo. Alikuwa namba moja kwa United msimu uliopita, lakini jeraha la misuli ya paja lilimfanya akose mechi za kujiandaa na msimu wa klabu hiyo.

Dirisha la usajili la Uturuki litafungwa leo Ijumaa, na kuna matarajio Onana, ambaye amemaliza vibaya pia majukumu ya kimataifa na taifa lake la Cameroon, anaweza kucheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Fenerbahce Jumapili.

Related Articles

Back to top button