Afrika Mashariki

Okwi atua Kiyovu ya Rwanda

MCHEZAJI wa zamani wa Simba na Yanga, Emmanuel Okwi amesajiliwa na Kiyovu Sports Club ya Rwanda kwa mkataba wa mwaka mmoja.

“Tunafuraha kuthibitisha kuwa mshambuliaji, Emmanuel Okwi amesaini mkataba wa mwaka mmoja. Karibu Okwi,” alisema mwenyekiti wa Kiyovu Sports, Juvénal Mvukiyehe katika taarifa yake.

Mbali na kuwa mchezaji muhimu wa timu ya taifa ya Uganda ambaye ni nahodha, Okwi amechezea klabu kadhaa nchi mwake na nje ya nchi hiyo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 hakuwahi kuichezea timu yoyote baada ya kuachana na klabu ya nchini Misri yenye makao yake jijini Alexandria ya Ittihad.

Akiwa Kiyovu Sports, Okwi atakutana na wachezaji wapya waliosajiliwa akiwemo mshambuliaji Mcongo, Pinoki Vuvu Patsheli kutoka AS Maniema de Kindu ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na beki Ndayishimiye Thierry kutoka Marines FC.

Okwi amewahi kuchezea klabu ya Uganda ya Sports Club Villa, pamoja na klabu mbili kubwa za Tanzania Simba na Yanga

pamoja na muda mfupi alitua katika klabu ya Tunisia ya Etoile Du Sahel na ya Denmark ya SønderjyskE Fodbold.

Okwi alicheza Ligi Kuu ya Uganda akiwa na SC Villa kabla hajajiunga na Simba Sports ya Tanzania kwa ada ya dola za Marekani 40,000.

Januari, 2013, timu ya Tunisia ya Étoile Sportive du Sahel ilimsajili Okwi kwa ada iliyokuwa rekodi Tanzania ya dola za Marekani 300,000, hata hivyo timu hiyo ilishindwa kulipa ada hiyo kwa Simba, lakini baadae Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) lilimtaka mchezaji huyo kurudi kuichezea Villa ya Uganda.

Pia aliwahi kuichezea Yanga kwa miezi kadhaa licha ya Simba kupinga.

Okwi alijiunga na Simba Agosti, 2014 kwa mkataba wa chini ya miezi sita, ikielezwa kuwa Yanga ilitengua mkataba wa mchezaji huyo baada ya kushindwa kulipa dola za Marekani 50,000.

Okwi alikataa kucheza mechi tato za mwisho za Yanga za msimu wa mwaka 2013–14 kwa sababu ya utata wa malipo.

Juni 2017, Okwi kwa mara ya tatu alisaini mkataba na Simba wa miaka miwili.

Julai mwaka 2019 baada ya kufanya vizuri katika fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon 2019), alijiunga na timu ya Ligi Kuu ya Misri ya Al Ittihad kwa mkataba wa miaka miwili.

Related Articles

Back to top button