
NAIROBI: MSANII maarufu wa muziki wa hip-hop nchini Kenya, Henry Ohanga, maarufu Octopizzo, ametangaza rasmi kuingia katika siasa na kugombea kiti cha Ubunge wa Kibra katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.
Kupitia video aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii, Octopizzo ambaye alikulia katika eneo la Kibra alieleza dhamira yake ya kuwakilisha jamii yake bungeni.
“Ni wakati wa kuwa na uongozi unaojali maskini, unaosimama kwenye misingi ya uadilifu, heshima, na fursa kwa watu wa Kibra,” alisema msanii huyo mwenye umaarufu mkubwa miongoni mwa vijana.
Octopizzo pia aliwahimiza vijana wenzake kutoshuhudia tu mabadiliko bali kujitokeza kugombea nafasi za uongozi, akisisitiza kuwa ni wakati wa kizazi kipya kushika usukani wa taifa.
Kibra ni mojawapo ya maeneo yenye wakazi wengi zaidi jijini Nairobi, na ni ngome yenye ushawishi mkubwa kisiasa. Kuibuka mshindi katika eneo hilo kutahitaji Octopizzo kubadilika kutoka kuwa ikon ya muziki hadi kuwa mtunga sera mwenye uwezo wa kushughulikia changamoto za wananchi.
Masuala kama ukosefu wa ajira kwa vijana, makazi duni, huduma za kijamii na maendeleo ya msingi ni baadhi ya mambo ambayo mara nyingi amekuwa akiyazungumzia kupitia muziki wake.
Tangazo hilo limezua mjadala mkali mitandaoni. Baadhi ya mashabiki wake wamelipongeza kwa uamuzi wa kishujaa, wakisema kuwa ni hatua ya mfano kwa vijana wanaotoka katika mazingira magumu kama Kibra.
Hata hivyo, wengine wameonyesha mashaka wakisema kuwa kuwa msanii maarufu hakumaanishi ana uzoefu wa kisiasa unaohitajika kuendesha shughuli za ubunge.
Wachambuzi wa siasa wanasema bado haijulikani kama mvuto wa jina la Octopizzo na ushawishi wake katika utamaduni wa vijana utaweza kutafsiriwa kutoka kwenye muziki kuingia kwenye siasa.
Octopizzo amefungua ukurasa mpya katika maisha yake, akibadilisha midundo ya hip-hop kuwa sauti ya mabadiliko ya kijamii. Wapiga kura wa Kibra sasa wanasubiri kuona kama nyota wao wa muziki ataweza pia kung’aa katika ulingo wa siasa.



