Nyota wa mieleka Wyatt afariki dunia

NYOTA wa mchezo wa mieleka Marekani, WWE Bray Wyatt amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 36 baada ya kuripotiwa kupata mshtuko wa moyo.
Afisa Mkuu wa Maudhui wa WWE Triple H ametangaza kifo cha Wyatt kupitia mtandao wa Twitter.
“Nimepokea simu hivi punde kutoka kwa baba mzazi wa Wyatt, Mike Rotunda ambaye ametuarifu kuhusu habari za kusikitisha kwamba mwanafamilia wetu wa WWE, Windham Rotunda – anayejulikana pia kama Bray Wyatt – amefariki bila kutarajiwa,”amesema Triple H.
Triple H amesema: “Mawazo yetu yako kwa familia yake na tunaomba kwamba kila mtu aheshimu faragha yake kwa wakati huu.”
Bingwa huyo mara tatu wa dunia wa WWE alikuwa hajashiriki mieleka tangu aliposhinda LA Knight katika mechi ya Mountain Dew Pitch Black kwenye Royal Rumble Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa ripoti za mtandao wa Fightful.com, Wyatt amefariki dunia baada ya kupata mshtuko wa moyo akiwa amepambania matatizo ya afya yake yaliyosababishwa na ugonjwa wa Covid-19 mapema mwaka huu.