NMB yakabidhi Bunge vifaa vya michezo

TIMU ya michezo ya Bunge imekabidhiwa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Sh milioni 20 na Benki ya NMB kwa ajili ya bonanza litakalofanyika Septemba 17 baina ya Bunge na benki hiyo huku kila upande ukijitapa kushinda.
Makabidhiano hayo yamefanyika bungeni kati ya Mwenyekiti wa timu ya Michezo ya Bunge na Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.
Tarimba akizungumza kabla ya kukabidhiwa vifaa hivyo alisema NMB kwa muda mrefu imekuwa wabia wa michezo bungeni na kuwa kwao ni faraja kwao na vifaa hivyo vimekuja kwa wakati.
“Tunafuraha mpango wenu wa bonanza maarufu kama ‘Kivumbi na Jasho’ baina ya NMB na Bunge, kwetu ni faraja na limekuja kwa wakati maana tunajiandaa pia kwa mashindano ya michezo ya mabunge ya Afrika Mashariki,” alisema.
Kwa mujibu wa Tarimba, bonanza hilo huwasaidia kujiandaa na kutoa mfano kuwa mwaka jana walishiriki bonanza hilo kwa mara ya kwanza na muda mfupi walikwenda kwenye mashindano ya mabunge ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Arusha mwaka jana na iliwasaidia kujinoa na kuibuka washindi.
“Katika mashindano hayo, Bunge la Tanzania lilishinda michezo yote nane na liliibuka mshindi wa jumla…tulishinda vikombe vingi, kwa kweli mlitusaidia kujinoa. Kwa hiyo hata kupitia bonanza hili litatusaidia kwani baadaye mwaka huu tunakwenda kushiriki mashindano tena ya mabunge ya Afrika Mashariki,” alisema na kuongeza kuwa wamefurahi kukabidhiwa vifaa hivyo.
Tarimba alisema michezo hiyo inawasaidia kutengeneza ushirikiano mzuri baina ya bunge na benki lakini pia wengi wao ni wateja wa benki hiyo.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Zaipuna alishukuru wabunge na ofisi ya bunge kwa ushirikiano na benki ya NMB.
Amesema bonanza hilo litakuwa na matukio kadhaa ikiwa ni pamoja na matembezi kuanzia Uwanja wa Chinangali hadi Hospitali ya Uhuru watakapokwenda kukabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 50.
Vilevile alisema baada ya bonanaza hilo pia jioni watakuwa na hafla ya mchapalo kwa lengo la kufurahi pamoja, kubadilishana mawazo na kudumisha ushirikiano.