Michezo MingineRiadha

NMB MARATHON 2022: Mbio kusaidia matibabu ya Fistula

MSIMU wa pili wa NMB Marathon, umepangwa kufanyika Septemba 24, 2022, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, lengo likiwa ni kukusanya kiasi cha Sh milioni 600 kusaidia matibabu ya akina mama wanaosumbuliwa na maradhi ya fistula kwenye Hospitali ya CCBRT.

Mbio ambazo zitashindaniwa katika Marathon hiyo ni zile za kilometa 5, 10 na 21 na washindi wanatarajiwa kuondoka na fedha taslimu pamoja na medali.

MAFANIKIO

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mbio hizo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Ruth Zaipuna anasema baada ya mafanikio katika mwaka wa kwanza wa mbio hizo, anaamini malengo ya miaka minne yatakamilishwa katika mbio za mwaka huu.

“Mwaka jana tulizindua mbio hizi za hisani kwa kaulimbiu ya Mwendo wa Upendo, ambayo mwaka huu tumeamua kwenda nayo hiyohiyo, lengo likiwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 1 katika kipindi cha miaka minne, kwa maana ya Sh milioni 250 kila mwaka,”

“Lakini tukapata mafanikio makubwa yaliyotuwezesha kukusanya Sh milioni 400, ambazo tulizipeleka CCBRT na kusaidia kina mama mbalimbali waliokuwa na tatizo la fistula. Mwaka huu, tumeona haja ya kuweka lengo la kukusanya Sh milioni 600 ili kutimiza Sh bilioni 1 ndani ya miaka miwili,” anasema Zaipuna.

Zaipuna anasema lengo ya kuanzisha mbio hizo ni kuendeleza dhamira mama ya benki hiyo ya kurudisha kwa jamii kwa kile cha ziada inachokipata katika shughuli zake za kuwahudumia Watanzania.

Kiongozi huyo anasema Benki ya NMB imekuwa mstari wa mbele kusaidia mambo mbalimbali, ikiwemo ya kijamii na michezo na kutokana na kuguswa na matatizo ya akina mama ya ugonjwa wa fistula ndio maana wameona kutoa mchango wao kama walivyokusudia.

“Tuna ushuhuda wa kutosha kuhusu kesi za baadhi ya akina mama wanaosumbuliwa na ugonjwa wa fistula na kwa kuwa lengo letu ni kuisaidia serikali tumeamua kuanzisha mbio hizi ili kupunguza unyanyapaa wa akina mama, ambao wanasumbuliwa na ugonjwa huo,” anasema Zaipuna.

Kiongozi huyo amewaomba wananchi na wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kushiriki mbio hizo sababu kufanya hivyo kuokoa mamia ya akina mama ambao ni wahanga wa ugonjwa huo.

Katika upande wa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi, anaishukuru NMB kwa kuliona tatizo hilo na kulisimamia kutaka kulimaliza kupitia makusanyo ya fedha za mbio hizo.

Msangi anasema tatizo la fistula ni kubwa sana Tanzania, ambapo kila mwaka zaidi ya akina mama 3,000 wanakumbwa na ugonjwa huo na wanashindwa kupata matibabu kwa wakati kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosa fedha na kuona aibu.

Anasema mwaka jana baada ya kufanyika kwa mbio hizo ilisaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha matibabu ya akinamama waliokuwa wanasumbuliwa na tatizo hilo, ambalo linasababisha wanawake wengi kutengwa na watu wao wa karibu.

“Sidhani kama kuna benki iliyowahi kutoa ahadi ya kusaidia Sh bilioni 1 ya matibabu ya fistula, tatizo hili ni kubwa nchini, kwani ukiondoa kina mama 3,000 wanaopata tatizo hilo kila mwaka, wapo wagonjwa wa zamani wanaoendelea kusumbuliwa na tatizo hili.

MATATIZO

“Kuna maeneo mawili yanayosababisha kina mama kuendelea kusumbuliwa na fistula, la kwanza likiwa ni elimu. Jamii haina elimu ya kutosha juu ya tatizo hili, kwamba bado tatizo hili halieleweki na jamii inawatenga wanawake wanaokumbwa na maradhi haya yanayohusishwa na imani za kishirikina,” anasema Msangi.

Msangi anasema kwamba, tatizo la pili ni gharama kubwa, kuanzia za usafirishaji wa wagonjwa kutoka waliko hadi hospitalini kwake, gharama za matibabu pamoja na malazi na chakula wakati wakiendelea na matibabu, hivyo NMB imeona mbali kusaidia kada hiyo muhimu katika jamii.

Msangi alibainisha kuwa, kupitia Sh milioni 400 za NMB Marathon 2021, CCBRT iliweza kupambana na changamoto hizo mbili zinazokosesha tiba kwa akina mama wenye fistula, ambazo ziligharamia tiba ya wanawake 60, pia zilitumika kuzunguka katika mikoa minne ya Rukwa, Kagera, Mtwara na Songwe kutoa elimu.

Kiongozi huyo amewaomba wana michezo, viongozi mbalimbali wa nchi kuitumia fursa hiyo kwa kushiriki mbio hizo kwa lengo la kusaidia matibabu ya akina mama hao ambao wanateseka na ugonjwa huo.

Kwa mara nyingine mtendaji wa NMB, Zaipuna anasema malengo ya Benki yao ni kuendelea kuipambania jamii ili kusaidia changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo masuala ya michezo na hiyo haitokuwa mara ya kwanza kwao.

KUENDELEA

Zaipuna anasema wataendelea kuandaa mbio hizo kila mwaka kutokana na makusudio mbalimbali na uhitaji au tukio husika sababu wameshawahi kujitambulisha hivyo kwa jamii tangu huko nyuma walipoanza kutoa huduma za kibenki.

“Tumewahi kudhamini timu mbalimbali za mpira wa miguu, kikapu, riadha, gofu na michezo mingine lengo letu ni kuisaidia Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinyanyua michezo nchini,” anasema Zaipuna.

ZAWADI NONO

Kiongozi huyo anasema kwa kuthamini mchango wa wale ambao watajitokeza kushiriki mbio hizo, benki ya NMB imeandaa zawadi maalumu zenye ubora wa hali ya juu ili kutambua mchango wao katika kulifanikisha na kupunguza tatizo hilo la ugonjwa wa fistula.

Zaipuna anasema zawadi hizo kwa washiriki zitakabidhiwa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa ambaye ndiye atakuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo kubwa nchini katika mbio za marathoni.

Related Articles

Back to top button