“Nitairejesha Italy” – Gattuso

MILAN: Kocha mpya wa timu ya taifa ya Italia Gennaro Gattuso ameahidi kurejesha ari na kuunda ‘familia’ katika timu hiyo ya taifa iliyoparaganyika akilenga kupata nafasi ya kufuzu Kombe lijalo la Dunia baada ya timu hiyo yenye jina la utani la Azzurri kukosa mara mbili mfululizo fainali hizo.
Gattuso anachukua nafasi ya Luciano Spalletti, ambaye alitimuliwa mapema mwezi huu kufuatia kichapo cha mabao 3-0 kutoka kwa Norway katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia na kuondoka rasmi baada ya mechi yake ya mwisho ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Moldova.
“Ni ndoto iliyotimia, na hakika ninatumai kulivaa vyema jukumu hili. Najua kazi haitakuwa rahisi, lakini hakuna kitu rahisi maishani,” amesema Gattuso, ambaye hivi karibuni aliihama klabu ya Hajduk Split ya Croatia, baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu katika ligi kuu ya nchi hiyo.
Akiwa amepewa jina la utani ‘Ringhio’ (Mkulima) kwa tabia yake ya kutumia nguvu nyingi uwanjani, mchezaji huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 47 aliichezea timu ya taifa ya Italia mechi 73 na alikuwa kiungo muhimu wa kikosi kilichoshinda Kombe la Dunia la 2006.
Mashabiki wanatumai nguvu yake hiyo inaweza kusaidia katika jukumu la kuwapeleka mabingwa hao mara nne wa dunia kwenye Kombe la Dunia la mwaka ujao, ambalo litachezwa Marekani, Mexico na Canada.
Italia, ambayo ni ya tatu katika Kundi I la kufuzu kwa Kombe la Dunia, itaikaribisha Estonia Septemba 5 kabla ya kumenyana na Israel siku tatu baadaye.
“Lengo langu ni kumfanya yeyote anayekuja kwenye uwanja wa mazoezi anakuja na shauku kubwa na kutengeneza familia,” alisema Gattuso, ambaye kwa mujibu wa chanzo cha ndani ya shirikisho la soka la Italia (FIGC) amepewa mkataba wa mwaka mmoja.
Gattuso alitumia muda wake mwingi wa uchezaji katika klabu ya AC Milan, ambapo alishinda Ligi ya Mabingwa mara mbili na mataji mawili ya Serie A, kabla ya kurejea kuifundisha klabu hiyo kuanzia 2017 hadi 2019. Akiwa meneja alishinda Coppa Italia akiwa na Napoli mwaka 2020.