Mwanamuziki wa taarabu afariki dunia

DAR ES SALAAM: MWANAMUZIKI mkongwe na mtunzi wa muziki wa taarabu nchini, Ally Hemed ‘Ally Star’ amefariki dunia leo, Februari 3, 2026 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa.
Ally Star ambaye amefanya kazi kwa muda mrefu akiwa na bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), alikuwa amelazwa Muhimbili kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Msanii huyo kabla ya umauti wake, aliwahi kusema kuwa amekuwa akipata mshtuko wa mwili unaofanana na kupigwa na umeme, hali iliyoanza katikati ya mwaka jana na kuendelea kuongezeka hadi kufikia hatua ya kulazimika kulazwa hospitalini.
Mkurugenzi wa T.O.T Khadija Kopa amethibitisha kutokea kwa msiba huyo: “Ally ni kweli amefariki baada ya kuugua muda mrefu, taratibu za mazishi zinaendelea,”
Ally Star ni mtunzi na mwimbaji mkongwe aliyeacha alama kubwa katika muziki wa Tanzania, hususan kupitia wimbo maarufu “Hauvumi Lakini Umo” uliopata umaarufu mkubwa mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Nyimbo nyingine alizotunga na kuimba ni pamoja na Zumbukuku na Limbukeni.
Katika safari yake ya muziki, Ally Star amewahi kuzitumikia bendi kadhaa maarufu zikiwemo Orchestra Safari Sound, Double O, Bima Modern Taarab na Tanzania One Theatre (TOT).
Mwisho




