Mwanamuziki wa kike akataa kujiunga na lebo za muziki Nigeria

LAGOS: MWIMBAJI mashuhuri nchini Nigeria aliyeshinda tuzo kadhaa za muziki, Niniola Apata, amefunguka kuhusu uamuzi wake wa kubaki huru kwa muongo mmoja, licha ya kupokea ofa nyingi kutoka lebo mbalimbali za muziki zikitaka ajiunge nao.
Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni na Hip TV, mwimbaji huyo anayetamba na wimbo wa ‘All Eyes On Me’ alieleza kuwa chaguo lake lilitokana na nia ya kulinda uhuru wake wa kisanii, hasa kwa sauti yake ya kipekee inayofanya mchanganyiko wa muziki wa Kiafrika, beats za nyumbani, na mtindo wake binafsi.
“Nimekuwa msanii wa kujitegemea kwa miaka 10 sasa, na ina faida na hasara zake,” amesema. “Baada ya kuachia wimbo wangu wa kwanza mwaka wa 2014, lebo kadhaa za rekodi zilinifikia, lakini nilikuwa na shaka kwa sababu sikutaka mtu yeyote aniondolee uhuru wangu wa ubunifu.”
Niniola alifichua kuwa wakati huo, Afrohouse haikuwa aina inayokubalika na wengi, na alihofia kuwa lebo zingemlazimisha kubadilisha muziki wake ili kuendana na mitindo ya kibiashara. Badala ya kusaini mkataba, alishirikiana na meneja wake wa zamani kuzindua lebo yao wenyewe.
“Hata kwa miaka mingi, mikataba kadhaa imekuja, lakini sijaridhika nayo,” ameongeza.
Niniola pia alielezea Afrohouse kama “mchanganyiko wa mtindo wa Kiafrika na muziki wa nyumbani,” akisisitiza kwamba ni ustadi wake binafsi ambao unafafanua sauti inayobadirika badirika. “Inajisikia vizuri kujulikana kama malkia wa Afrohouse,” amesema.
Mwimbaji huyo, ambaye anaimba sana Kiyoruba, alibainisha kuwa uhalisi na uthabiti wake umemsaidia kuwa na mashabiki waaminifu licha ya shaka ya awali kuhusu maisha marefu ya muziki wake.
“Mwisho wa siku, nimeona kwamba unahitaji tu kuwa wewe mwenyewe, kuomba, kuwa na shukrani, na kila kitu kitakuwa sawa,” amehitimisha Niniola.