Nyumbani

Mwana FA azichana makavu Simba, Yanga

DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamisi Mwinjuma ( Mwana FA), ametoa wito mzito kwa viongozi wa klabu kubwa hapa nchini, akiwasihi wahamasishe utekelezaji wa mipango yao badala ya kubaki katika makaratasi na maneno matupu.

Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla ya kumtambulisha mzabuni mpya wa klabu ya Simba, Mwana FA amesema ni muda wa vitendo sasa, hususan katika suala nyeti la ujenzi wa viwanja vya kisasa.

“Sasa ni muda wa kutoka kwenye makaratasi na kuingia vitendo. Uwanja bora wa kuchezea mechi za ligi si tu utapunguza mzigo kwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, bali pia utainua hadhi ya klabu,” amesema kwa msisitizo.

Kwa furaha na matumaini, Mwana FA aliipongeza Simba kwa kupata mzabuni mpya , ambaye ameahidi kuujenga uwanja wa kisasa eneo la Bunju, pamoja na kuweka miundombinu muhimu kama basi la timu, vyumba vya matibabu, na ofisi bora kwa wanahabari – hatua ambayo alisema inaleta taswira ya klabu ya kimataifa.

“Ninaamini utaratibu wa kumpata mzabuni huyu ulikuwa wa haki na unaolenga maendeleo ya kweli. Tumeusubiri mradi huu kwa muda mrefu, sasa tuone matokeo,” amesema Mwana FA.

Aidha, ameeleza dhamira ya serikali kuhakikisha Tanzania inakuwa na viwanja vingi na bora, huku akiahidi kuwa hawatamuangusha Rais Samia Suluhu Hassan katika juhudi zake za kuleta mapinduzi kwenye sekta ya michezo.

Katika kuhitimisha, Mwana FA ameipongeza Simba kwa hatua ya kufika nusu fainali ya michuano ya kimataifa na kuwatia moyo kuelekea mechi yao dhidi ya Stellenbosch, Zanzibar Aprili 20, na ile ya marudiano Aprili 27 nchini Afrika Kusini.

“Kauli mbiu yao imetoka ‘Hii tunavuka’ hadi ‘Hatuishii hapa’. Nina imani watavuka na kufika fainali. Serikali ipo nyuma yao bega kwa bega,” amesisitiza.

Kwa ujumla, hotuba ya Mwana FA ilikuwa ni mwito wa kuchukua hatua, kujenga misingi ya maendeleo ya kudumu, na kuinua kiwango cha mpira wa miguu nchini kwa vitendo na si maneno pekee.

Related Articles

Back to top button