
DAR ES SALAAM:MSANII wa kwanza wa kike kutoka lebo ya Kings Music Records, Mutimawangu, amewasili nchini Tanzania akitokea nchini Rwanda, ambapo kwa mara ya kwanza tangu atue amezungumza na waandishi wa habari kueleza hisia zake baada ya kutambulishwa rasmi kama msanii mpya wa lebo hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mutimawangu amesema safari yake hadi kufikia hatua ya kutambulishwa haikuwa rahisi, kwani amekaa benchi kwa muda wa miaka minne akisubiri kusajiliwa na kupewa nafasi rasmi chini ya lebo ya Kings Music.
“Nadhani kutambulishwa kama msanii wa kwanza wa kike wa lebo ya Kings Music kwangu ni baraka kubwa. Haikuwa rahisi, nimekaa muda mrefu kusubiri kutambulishwa, lakini naamini huu ulikuwa wakati sahihi,” amesema Mutimawangu.
Kwa upande wake, msanii na mmiliki wa lebo ya Kings Music Records, Ali Kiba, amesema kuwa uamuzi wa kumtambulisha Mutimawangu umefikiwa baada ya kuona ni muda muafaka, licha ya changamoto zinazowakumba wasanii wa kike katika safari yao ya muziki.




