Mtanzania ang’ara Tuzo za Kwanza za TikTok 2025

JOHANNESBURG: MOJA ya matukio yaliyosubiriwa kwa hamu kubwa mwaka huu ni pamoja na Tuzo za TikTok Afrika zilizofanyika kwa mafanikio makubwa katika jiji la Johannesburg nchini Afrika Kusini.
Tuzo hizo zinadaiwa kuibua vipaji, kuburudisha na kuthibitisha ukuaji wa upeo wa ubunifu barani Afrika licha ya kufanyika kwa mara ya kwanza.
Muigizaji kutoka Tanzania Fanuel Masamaki anayeigiza kwa kucheza mpira na anapofunga huruka kama ronado kwa kusema neno Suuuuuu!!! Ameshinda kipengele cha Video Bora ya Mwaka.
Masamaki, mwenye miaka 26, aling’ara kwa maudhui yake ya kusisimua yanayoburudisha soka kwa ubunifu mkubwa na hivyo kuiletea Afrika Mashariki ushindi wa kifahari.
Katika kipengele hicho Fanuel Masamaki kutoka Tanzania alishindana na David Mubiru kutoka Uganda na mchekeshaji wa Nigeria Isaac Samz.
Katika tuzo hizo burudani iliongozwa na mwanamuziki chipukizi kutoka Afrika Kusini Ciza Isaka anayetamba katika muziki wa Afrika Mashariki, hasa Kenya, kupitia kibao chake ‘Isaka’ aliowashirikisha wanamuziki Jazzwork na Thukuthela.
Wimbo huo uliibua challenge ya dansi barani kote miezi sita iliyopita, ukikusanya zaidi ya video milioni mbili na kushika nafasi ya tatu kati ya nyimbo maarufu za majira ya kiangazi zinazotamba kwenye mtandao wa TikTok Afrika Kusini.
Katika tuzo hizo, Ciza alipanda jukwaani na kutoa shoo ya dakika 10 iliyowafanya mashabiki na wageni mashuhuri kumtaka mwanamuziki huyo mwenye miaka 24 arudie na kuimba zaidi.
Kwa zaidi ya watumiaji milioni 189 barani Afrika wanaotumia mtandao wa TikTok nchi za Nigeria, Afrika Kusini na Kenya ndizo zilizotawala usiku huo kutokana na idadi kubwa ya watumiaji wa mtandao huo na ushiriki wao katika usiku huo wa tuzo.
MwanaTikTok kutoka Nigeria, Belove Olocha alishinda tuzo mbili ikiwemo ya Mwandishi Bora wa Mwaka wa Simulizi na Mburudishaji Bora wa Mwaka.
Roy Kanyi na Mutisya Musyoki kutoka Kenya wameshinda kipengele cha Maudhuri Bora ya Elimu na Nafasi za juu mbili zilichukuliwa na Mitchell Tafadzwe kutoka Afrika Kusini na Izzi Boye wa Nigeria.
Wengine walioshinda kutoka Kenya ni Boyz Makekii (Arnold Mbayi) akishinda tuzo ya Mbunifu Bora wa Chakura wa Mwaka huku John Mbugua akishinda tuzo ya Mbunifu Bora wa Michezo wa Mwaka.




