Mtanzania afikisha mechi 100 Mexico

MEXICO: MWANASOKA wa kimataifa wa Tanzania, Julitha Singano, ameweka rekodi ya kihistoria katika klabu yake ya FC Juárez Femenil ya nchini Mexico, baada ya kufikisha jumla ya michezo 100 tangu alipojiunga na timu hiyo mwaka 2022 akitokea Simba Queens ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi za klabu hiyo, Singano amekuwa miongoni mwa wachezaji wachache wa kigeni walioweza kufikisha idadi hiyo ya mechi katika kipindi kifupi, jambo linaloonesha uimara na mchango wake ndani ya timu.
Wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo ulimpongeza Julitha kwa rekodi hiyo kupitia akaunti ya timu ya mtandao wao wa kijamii.

Tangu atue Mexico, Singano amecheza mechi hizo kwa msimu kama ifuatavyo:
2022–2023: Michezo 14
2023–2024: Michezo 38
2024–2025: Michezo 33
2025–2026: Michezo 15 (hadi sasa)
Nyota huyo wa zamani wa Ligi Kuu amejizolea kadi za njano 22 na kadi nyekundu nne , akionesha nidhamu na ushindani mkubwa uwanjani.
Mafanikio hayo yamemfanya kuwa mchezaji wa kwanza Mtanzania kufikisha idadi hiyo ya mechi katika ligi ya wanawake ya Mexico, na moja ya wachezaji wanaowakilisha vyema bara la Afrika katika soka la wanawake la Amerika ya Kati.




