Mavazi

Miriam Odemba: Anko Hashim Lundenga aandikiwe kitabu cha maisha yake

DAR ES SALAAM: MSHINDI wa Shindano la kisura wa Afrika 1998 na Miss Earth Air 2008, Miriam Odemba amesema ili kumuenzi kwa vitendo Mratibu wa zamani wa mashindano ya Miss Tanzania, Hashim Lundenga ‘Anko Lundenga’ inafaa kiandikwe kitabu kuhusu maisha yake hadi kifo kwa ajili ya kumbukumbu kwa tasnia ya urembo na vizazi vijavyo.

Hashim Lundenga amefariki dunia Jumamosi Apili 19, 2025 katika Hospitali ya Itengule, Tegeta Jijini Dar es Salaam na mwili wake umezikwa Aprili 22,2025 katika makaburi ya familia huko, Kidatu mkoani Morogoro.

Odemba amefafanua namna kitabu hicho kitakavyoandikwa kwa kushirikiana na Kamati ya Miss Tanzania, makala na habari zinazomuhusu Anko Lundenga zikusanywe kisha atafutwe mwandishi nguli anayemfahamu vyema Anko Lundenga ili aandike kitabu hicho kitakakuwa kumbukumbu ya kweli kwa tasnia ya urembo.

“Tumempoteza mtu muhimu mno kwenye tasnia ya urembo Anko Hashim alikuwa mtu mwema sana…..alikuwa anasikiliza kila tatizo la miss na alikuwa anajua nini maana ya Umiss! Kwakweli tumempoteza Shujaa wa Urembo na Tutamkumbuka daima. Ulikuwa ukimuona Hashim lundega umeona Miss Tanzania, tuendelee kumuenzi kwa kufanya kitu kikubwa kiwe kumbukumbu yetu kwake kama kumuandikia kitabu kuhusu maisha yake,” ameeleza Odemba.

Odemba ameongeza: “Tuzidi kuenzi mazuri yake tusisahau mazuri aliyofanya Katika Tasnia ya Urembo bila Hashimu lundenga tusingekuwa na Miss Tanzania. Mimi kama mimi nimeumia sana kwangu alikuwa Baba, Anko na Mentor wangu.”

Back to top button