Miradi 18 yatekelezwa sekta ya michezo

DODOMA: KATIKA kipindi cha utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, Serikali imeendelea kutekeleza programu na miradi 18 yenye lengo la kuongeza mchango wa sekta katika ukuaji wa uchumi na ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2024 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2025/26.
Amesema katika kufikia lengo hilo, shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa viwanja kwa ajili ya mashindano ya AFCON; ujenzi wa vituo vya michezo na vituo vya kupumzikia wananchi; ujenzi wa vituo vya umahiri vya michezo, kuanzishwa kwa bodi ya ithibati ya wanahabari, utoaji wa mikopo kwa kazi za sanaa na utamaduni na kukuza Kiswahili Kikanda na Kimataifa.
Amesema mafanikio yaliyopatikana kutokana na utekelezaji wa shughuli hizo ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya miundombinu ya michezo iliyoboreshwa nchini kote kutoka 68 mwaka 2023/24 kufikia 174 mwaka 2024/25; kuongezeka kwa idadi ya wanariadha wanaocheza nje ya nchi kutoka 17 mwaka 2023/24 kufikia 62 mwaka 2024/25;
Pia, amesema kuongezeka kwa mchango wa sekta ya sanaa, michezo na ubunifu katika pato la taifa na kufikia asilimia 0.4; kuongezeka kwa ubora na ubunifu wa kazi za utamaduni na sanaa; kuongezeka kwa vipaji na kuongeza ushindani kimataifa, kuongezeka kwa utoaji wa habari kwa umma; kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari kwa kusajili na kutoa leseni.