Michezo Mingine

Michuano ya Kriketi ya Caravan kuzinduliwa leo

DAR ES SALAAM: MASHINDANO ya 16 ya Petrofuel TCA Caravans Cup 2025 yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi leo Dar es Salaam katika sherehe maalum itakayofanyika usiku kwenye Hoteli ya Sea Cliff.

Akizungumza kuelekea uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Caravans Cricket Club, Thulasee Das, amesema mashindano ya mwaka huu ni makubwa zaidi kwa historia ya Caravans Cup na yataendeshwa kwa ushirikiano wa karibu na Shirikisho la Kriketi Tanzania (TCA).

Alibainisha kuwa mashindano haya ni jukwaa muhimu kwa wachezaji wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo wanaotoka India, Pakistan, Sri Lanka, Zimbabwe na Uingereza.

Mashindano yataanza rasmi Juni 28, 2025 na kumalizika Agosti 10, mwaka huu katika uwanja wa kihistoria wa Dar es Salaam Gymkhana Club. Mfumo wa ligi ya mzunguko utatumika, ambapo kila timu itacheza na nyingine zote, kabla ya hatua ya mtoano kwa timu nne bora.

Mabingwa watetezi wa mashindano haya ni Alliance Caravans, huku Caravans Cricket Club ikishikilia rekodi ya kuwa klabu iliyotwaa ubingwa mara nyingi zaidi tangu kuanzishwa kwa mashindano haya. Timu nyingine zinazoshiriki ni Aurobindo AKSC, Flashnet Aces, Harab Motors Pak Stars, Park Mobile Lions, Raah Upanga Club, Jiuzhou Patel Samaj na KX Intek Gymkhana.

Mashindano haya yanaungwa mkono na wadhamini mbalimbali wakiongozwa na Petrofuel (T) Limited kama mdhamini mkuu. Wadhamini wa Platinum ni Alliance Insurance, ASAS, Automark, Ras Logistics na Pepsi, huku kila timu ikiwa na mdhamini wake wa franchise kama vile Aurobindo, Flashnet, e-Parking, Harab Motors, Jiuzhou, Raah Holdings na wengine.

Mbali na ushindani wa uwanjani, Caravans Cricket Club imetangaza pia kampeni mbili muhimu za kijamii. Ya kwanza ni kampeni ya uchangiaji damu kwa ushirikiano na Hospitali ya Taifa Muhimbili na Lions Club, na ya pili ni kampeni ya upandaji miti, ambapo mti mmoja utapandwa kwa kila “mpaka”, na miti 20 kwa kila “msimu.

Das alisisitiza kuwa mashindano haya yataendelea kuwa bure kwa watazamaji, hivyo kuwaalika mashabiki wa rika zote, familia na wapenzi wapya wa mchezo huo kufurahia kriketi ya hali ya juu.

Related Articles

Back to top button