Featured

Michezo yenye historia ya kipekee miaka 61 ya Uhuru

TANZANIA imetimiza miaka 61 tangu ilipopata uhuru wake mnamo Desemba 9, 1961.

Uhuru huu ulitokana na jitihada kubwa zilizoongozwa na muasisi wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akishirikiana na viongozi wengine ambao walipigana kwa nguvu zao zote kuhakikisha uhuru unapatikana.

Michezo ni sehemu ya mafanikio ya uhuru huo kwani nchi imepiga hatua kubwa pia katika eneo hilo kama ilivyo katika nyanja za uchumi na huduma za jamii.

Serengeti Girls

Oktoba mwaka huu timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Girls ilicheza Fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake zilizofanyika nchini India kuanzia Oktoba 11 hadi 30.

Maendeleo ya juu kabisa kufikiwa katika mpira wa miguu kwa Tanzania kuwa na mwakilishi katika fainali hizo za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) zilizoshirikisha timu 16 kutoka katika mabara yote duniani.

Tanzania ilikuwa moja kati ya nchi tatu zilizoiwakilisha Afrika, timu nyingine kutoka Afrika
zilikuwa ni Nigeria na Morocco.

Uwakilishi wa timu hizi kwa Afrika ulikuwa mzuri, kwani wakati Morocco ikitolewa katika hatua ya makundi Tanzania ilicheza robo fainali na Nigeria
ilifika hatua ya nusu fainali na kumaliza katika nafasi ya tatu.

Katika fainali hizo, Tanzania na Nigeria zote zilitolewa na Colombia ambayo ilishika nafasi  ya pili na Hispania ikifanikiwa kutetea ubingwa wake tena. Kwa hatua ambayo Serengeti Girls imefikia, inaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa timu 16 bora duniani kwa mpira wa
miguu wa wanawake kwa umri chini ya miaka 17.

Serengeti Girls ilikuwa katika kundi D pamoja na timu za Japan, Ufaransa na Canada na iliwavutia wengi kwani wachezaji zaidi ya sita waliwavutia mawakala mbalimbali na baadaye wakifikisha miaka 18 watakuwa na nafasi ya kwenda kucheza soka Ulaya na sehemu nyingine ambapo kisheria ndipo wanaweza kusaini mikataba ya ajira.

Tembo Warriors

Kwa kuonesha kuwa Tanzania inaheshimu usawa na kuwapa nafasi ya
kucheza timu ya walemavu ya mpira wa miguu ilishiriki Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Uturuki kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 5 mwaka huu.

Mwalimu Nyerere katika mojawapo ya nukuu zake aliwahi kusema: “Maendeleo ni yetu na ni juu yetu wenyewe, yataletwa na watu, yaendeleze watu, yawafae watu.”

Nukuu hiyo inaonesha jinsi ambavyo Tanzania kila mtu anashiriki kuleta maendeleo kwa nafasi yake kama ambavyo walemavu walivyoshiriki fainali za Kombe la Dunia na kufanikiwa kufika hatua ya robo fainali.

Simba na Yanga

Kwa upande wa klabu ya Simba imefanya vizuri katika vipindi mbalimbali
na kufanikiwa kuiwezesha kuwa na wawakilishi wanne katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Simba imefanikiwa kufika robo fainali hatua ambayo imeifanya kuwa miongoni mwa timu zinazoogopwa katika mashindano ya Caf na safari hii imefanikiwa kutinga hatua ya makundi sasa inangoja kujua itakutana na nani kwenye Ligi ya Mabingwa.

Pia klabu ya Yanga nayo inafanya vizuri na imetinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho. Riadha Mchezo wa riadha una historia ya kipekee katika nchi hii kwani wanariadha wake wamefanikiwa kuandika historia za kipekee na nyingine hazijavunjwa
hadi leo.

Filbert Bayi mkimbiaji wa zamani wa mbio za masafa ya kati aliweka rekodi ya dunia ya mita 1,500 michezo ya Jumuiya ya Madola mwaka 1974 yaliyofanyika Christchurch,
New Zealand, ambayo hadi 2022 haijavunjwa.

Pia aliwahi kushika nafasi ya kwanza katika mashindano ya All African Games mwaka 1973 na 1978 katika mbio za mita 1,500.

Juma Ikangaa ambaye alikuwa anakimbia mbio za marathon alishinda New York City Marathon mwaka 1989 kwa muda wa saa 2:08:01 na katika mbio za Boston Marathon alimaliza katika nafasi ya pili kwa miaka mitatu mfululizo katika mbio za Boston Marathon kati ya mwaka 1988-1990.

Suleiman Nyambui aliyebobea katika mbio za masafa marefu alishinda medali ya shaba katika Michezo ya All-Africa ya 1978, medali ya fedha katika mbio za mita 5,000 katika
Olimpiki ya majira ya joto ya 1980 na kumaliza wa kwanza katika marathon tatu mfululizo kati ya 1987 na 1988.

Ukiachana na wakongwe hawa watatu ambao waliiweka Tanzania katika ramani ya nchi zenye wanariadha hatari sasa kuna mkiambiaji mwingine anaitwa, Felix Simbu. Simbu (alizaliwa Februari 14, 1992), ni mwanariadha wa mbio ndefu ambaye amebobea katika
mbio za marathon.

Mwaka 2015 alishiriki katika Mashindano ya Dunia ya Riadha huko Beijing, China akamaliza wa 12 kwa muda wa saa 2:16:58. Katika michezo ya Olimpiki ya majira ya joto ya mwaka 2016 katika mbio za marathoni alimaliza wa tano kwa muda wa 2:11.15.

Mwaka 2017 alishinda medali ya shaba katika Marathon ya Mabingwa wa Dunia kwa muda wa saa 2:09:51. Aliwakilisha Tanzania katika michezo ya Olimpiki ya majira ya joto ya mwaka 2020 ambapo alipata nafasi ya 7 kwa muda wa saa 2:11:35.

Alishinda medali ya fedha katika Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 2022 katika mbio za marathoni za wanaume.

Pia yupo Gabriel Geay, ni mkimbiaji wa mbio ndefu na nusu marathoni ambapo hadi sasa ameshinda mbio saba mashuhuri za barabarani ikiwa ni pamoja na mbio za barabara za Peachtree (2016) na Bolder Boulder km 10 (2017) na juzi alishika nafasi ya pili katika mbio za km 42 zilizofanyika huko Valencia, Hispania na kuweka rekodi yake mpya ya 2:03:00.

Ngumi

Kwa upande wa ngumi nazo zimeipeperusha vema bendera ya Taifa ambapo kwa sasa Twaha Kiduku na bondia kutoka Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Seleman Kidunda ndio wanaofanya vizuri kimataifa.

Pia kwa upande wa michezo ya jadi mchezo wa kukuna nazi umetwaa kombe la dunia na kuitangaza vema nchi.

Tamasha Bagamoyo/ ZIFF

Tamasha la ZIFF linalofanyika kila mwaka visiwani Zanzibar limesaidia sana kuitangaza nchini kutokana na ujio wa wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali.

Aidha, Tamasha la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo nalo limekuwa kinara wa kuitangaza nchi kwani kila mwaka kumekuwa na maboresho na ongezeko la washiriki ambao ni wasanii
wa kimataifa.

Tamasha hilo hufanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).

Related Articles

Back to top button