
KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema atatumia siku zilizobaki kuimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ili iweze kufanya vizuri kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola.
Akizungumza na Spotileo Mgunda amesema siku za karibuni safu hiyo imekuwa na madhaifu ya kutumia nafasi inazotengeneza hivyo lazima ahakikishe anaiweka sawa kabla la mchezo huo.
“Maandalizi yetu yanakwenda vizuri ikiwa ni pamoja na kurekebisha mapungufu yetu yaliyojitokeza kwenye baadhi ya mechi za ligi na za kirafiki tulizocheza karibuni kitu cha msingi ni kuhakikisha tunatumia kila nafasi tutakayopata kwenye mchezo wetu na Primeiro de Agosto,” amesema Mgunda.
Amesema amefurahi wachezaji wameendelea kujituma kwenye mazoezi na kushika anachowaelekeza jambo linalompa matumaini ya kufanya vizuri kwenye michuano yote wanayoshiriki kwa sasa.
Simba leo itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Kipanga kwenye uwanja wa Amani, Zanzibar kisha kirejea Dar es Salaam kucheza mchezo mmoja wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji kabla ya kwenda Angola kuikabili Agosto.