
DAR ES SALAAM: KATIKA kile kinachoonekana kuwa ni matokeo ya mvutano mkali uliotokana na sintofahamu ya upangaji wa mechi ya Kariakoo Derby, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza mabadiliko makubwa ndani ya Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB).
Taarifa rasmi iliyotolewa na TFF kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Wilfred Kidao, imeeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto, amejiuzulu wadhifa wake kufuatia mvutano wa muda mrefu kuhusu upangaji wa mchezo huo namba 184 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Katika hatua nyingine, Rais wa TFF, Wallace Karia, amemsimamisha kazi Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo, hiyo ni baada sakata hilo linalohusisha mabadiliko ya tarehe ya mechi hiyo kubwa inayozikutanisha klabu kongwe za Simba na Yanga.
Mvutano huo ulianza baada ya klabu ya Yanga kueleza kutoridhishwa na maamuzi ya TPLB, ikiwemo kuhamishwa kwa tarehe ya awali ya mechi hiyo ambayo ilikuwa ipigwe Machi 8, lakini baadaye ikaahirishwa bila maelezo ya kina yanayoeleweka kwa pande zote.
Baada ya sintofahamu hiyo kuendelea kushika kasi na klabu ya Yanga kuonesha kutokuwa na imani na viongozi hao, hatimaye mchezo huo ulipangwa tena kufanyika Jumapili, Juni 15, kabla ya kusogeza mbele tena hadi Juni 25, huku ukiendelea kuibua hisia kali kwa mashabiki na wadau wa soka nchini.
Hatua ya Mguto kujiuzulu na Kasongo kusimamishwa ni ishara kwamba TFF inalenga kurejesha imani ya wadau na kuhakikisha uwazi katika upangaji wa ratiba, hasa kwa michezo mikubwa yenye mvuto kama Kariakoo Derby.
Kwa sasa, macho ya wadau yakielekezwa kwenye mchezo huo wa kiporo uliopangwa kuchezwa Juni 25 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.