Kwingineko

Messi awaka Argentina ikiifumua Puerto Rico 6-0

FORT LAUDERDALE: NAHODHA wa kikosi cha timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi usiku wa kuamkia leo ameisaidia timu yake kwa kuisambaratisha Puerto Rico mabao 6-0 kwa kutoa asisti mbili na kuanzisha shambulizi lililopelekea bao jingine, huku mabingwa hao wa Dunia, wakiibuka na ushindi huo katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliopigwa Jumanne usiku.

Mchezo huo awali ulipangwa kuchezwa Jumatatu mjini Chicago nchini Marekani, kabla waandaaji kuuhamishia katika uwanja wa Chase mjini Florida. Maafisa wa Chicago walitaja mauzo duni ya tiketi kama sababu kuu ya kuhamishwa huko, huku maafisa wa Shirikisho la Soka la Argentina wakiitaja kamatakamata wahamiaji mjini Chicago kama sababu.

Akiwa anacheza katika uwanja anaouita nyumbani akiwa na Inter Miami kwenye ligi kuu ya Marekani Major League Soccer, Messi alipiga mpira wa juu kwa ustadi mkubwa mpira uliomwezesha Gonzalo Montiel kufunga bao la kwanza katika kipindi cha kwanza, kisha akapiga pasi maridadi ya kisigino iliyopelekea Lautaro Martínez kufunga bao lake la pili dakika ya 83.

Alexis Mac Allister alifunga mabao mawili kwa timu yake ya taifa ya Argentina, ambayo pia ilinufaika na bao la kujifunga kutoka kwa mchezaji Steven Echevarria wa Puerto Rico katikati ya kipindi cha pili.

Kulikuwa na mazingira yaliyopelekea mchezo huo kuhamishwa kufuatia uwepo wa msako mkali wa wahamiaji uliosababisha zaidi ya watu 1,000 kukamatwa tangu mwezi uliopita katika eneo la Chicago.

Tiketi ziliuzwa saa chache kabla ya mchezo kwa bei ya chini ya dola 25, jambo ambalo ni nadra kwa mchezo wowote unaomhusisha Messi. Uwanja ulikuwa nusu wakati wa kuanza kwa mchezo, ingawa ulianza kujaa zaidi kadri dakika zilivyozidi kusogea.

Related Articles

Back to top button