Messi ajifunga Inter Miami hadi 2028

NEW YORK: GWIJI wa soka duniani na mshindi mara nane wa tuzo ya Balon d’Or, Lionel Messi, ameongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu ya Inter Miami ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS) hadi mwaka 2028.
Messi, mwenye umri wa miaka 38, hapo awali alinukuliwa akisema Inter Miami ingekuwa klabu yake ya mwisho kuitumikia katika maisha yake ya soka, lakini hajaashiria lolote kuhusu kuwa na mpango wa kustaafu hivi karibuni.
“Maono yetu yalikuwa kuwaleta wachezaji bora Inter Miami na katika jiji hili, na ndivyo hasa tumefanya. Messi bado anajitoa kama zamani na bado ana njaa ya ushindi na mafanikio hata katika nyakati hizi ambazo unaweza kusema anamalizia soka lake.” – amesema David Beckham, mmiliki mwenza wa klabu hiyo.

Nahodha huyo wa Argentina aliyeiongoza nchi yake kutwaa Kombe la Dunia 2022, anaongoza orodha ya wafungaji wa MLS kwa mabao 29 msimu huu, akisaidia Inter Miami kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo Ukanda wa Mashariki.
Tangu ajiunge na Inter Miami mwaka 2023, Messi ameleta msisimko mpya katika soka la Marekani, wakati huu ambao Marekani, Canada, na Mexico zinajiandaa kuwa wenyeji wa Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa jarida la Forbes, thamani ya Inter Miami imeongezeka maradufu tangu mwaka 2022 na kufikia dola bilioni 1.2, ikiwafanya kuwa timu ya pili yenye thamani kubwa zaidi katika MLS mwaka huu.
Miami wanatarajiwa kuvaana na Nashville SC katika raundi ya kwanza ya mechi za mtoano za Kombe la MLS kuanzia Ijumaa hii. Messi alitajwa pia miongoni mwa wachezaji watano walioteuliwa kuwania tuzo ya MVP ya msimu huu.




