Messi aingia kwenye historia afikisha mabao 900

MIAMI, Marekani: NYOTA wa soka duniani, Lionel Messi, ameingia rasmi kwenye kundi la wachezaji wachache waliofunga mabao 900 katika maisha yao ya soka, akimfuata mpinzani wake wa muda mrefu, Cristiano Ronaldo.
Messi alifikisha bao lake la 900 baada ya kufunga katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 bora dhidi ya Nashville SC uliochezwa Machi 18, 2026 katika Uwanja wa Chase, uliopo Fort Lauderdale, Marekani.
Hata hivyo, bao hilo halikuweza kuisaidia timu yake kusonga mbele baada ya kuondolewa kwenye michuano ya CONCACAF Champions Cup, mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 1-1, matokeo yaliyoifanya Nashville kufuzu hatua ya robo fainali kwa faida ya bao la ugenini kufuatia sare ya jumla ya 1-1 katika michezo miwili.
Katika mchezo huo, Messi aliandika historia kwa kufikia idadi hiyo kubwa ya mabao, lakini Cristian Espinoza aliibuka shujaa kwa upande wa Nashville baada ya kufunga bao muhimu kipindi cha pili lililohakikisha timu hiyo inatinga hatua inayofuata.
Kwa mujibu wa takwimu za Opta, Messi ameonesha ubora wa hali ya juu katika ufungaji, ambapo kati ya mabao hayo 900, amefunga 755 kwa mguu wake wa kushoto, 111 kwa mguu wa kulia, mabao 30 kwa kichwa na manne yakihesabika kama ‘mengineyo’.
Aidha, amefunga mabao 724 akiwa ndani ya eneo la hatari na 176 nje ya boksi, huku akifunga penalti 112 na mabao 70 ya mipira ya adhabu (free-kick).
Messi na Ronaldo, ambao kwa pamoja wameshinda Ballon d’Or mara 13, ndio wachezaji pekee katika historia ya soka ya wanaume kufikisha mabao 900.
Kwa upande mwingine, gwiji wa Brazil, Pelé, aliwahi kudai kufunga zaidi ya mabao 1,000, ingawa takwimu rasmi zinaonesha alifunga 778, huku Romário akitajwa kuwa na mabao 785.




