“Mechi na Bafana Bafana ni kama fainali” – Kocha Zambia

GQEBERHA: KOCHA mpya wa timu ya taifa ya Zambia (Chipolopolo), Moses Sichone, amesema mchezo wa kirafiki wa Jumamosi dhidi ya timu ya taifa ya Afrika Kusini (Bafana Bafana) utakuwa kama fainali kwake, anaposhika rasmi mikoba ya ukocha wa Chipolopolo ikiwa imebaki zaidi ya mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) nchini Morocco.
Sichone amechukua nafasi ya Avram Grant aliyefutupiwa virago nje baada ya kampeni duni ya kufuzu Kombe la Dunia, na anataka kuanza kwa ushindi ili kuleta ari mpya kambini mwa timu hiyo yenye taji moja la AFCON.
“Tunatarajia mchezo mgumu dhidi ya Afrika Kusini, lakini hatuendi kwa ajili ya kucheza tu. Tunauchukulia mchezo huu kwa uzito mkubwa kwa sababu tunataka kushinda ushindi wa heshima”
“Afrika Kusini wamefuzu Kombe la Dunia, kwa hiyo hii ni kipimo kizuri kwetu. Mimi nauona mchezo huu kama fainali.” – amsema Sichone.

Kocha huyo mpya amesema bado hajakamilisha kikosi chake cha mwisho kitakachokwenda Morocco kwa ajili ya AFCON, akisisitiza kuwa nafasi zipo wazi kwa wachezaji wote wanaofanya vizuri.
“Mlango bado uko wazi. Wachezaji wanaofanya vizuri kwenye ligi ya ndani bado wana nafasi. Tunajaribu kuchanganya wachezaji wenye uzoefu na vijana wapya. Kinachotakiwa ni moyo wa uzalendo wale walio tayari kufa kwa ajili ya nchi yao,” – aliongeza.
Sichone, ambaye aliwahi kucheza Bundesliga na kushiriki AFCON mara tatu akiwa mchezaji, sasa anapata nafasi yake kubwa ya kwanza kama kocha mkuu.
“Nimekuwa kwenye soka muda mrefu, nikiwa mchezaji na sasa kocha. Ni heshima kubwa kupewa nafasi hii. Najua si suala la kujionesha, bali ni uwakilishi wa watu milioni 20 wa Zambia,” alisema kwa unyenyekevu.
Akitambua shinikizo la matokeo kutoka kwa mashabiki, Sichone amesema “Mashabiki wanataka matokeo, lakini tusisahau tumepitia nyakati za kupanda na kushuka. Tutajitahidi kufanya kila tuwezalo kuhakikisha tunacheza vizuri na kuleta matumaini mapya.”
Zambia na Afrika Kusini zote zinatumia mechi hii kama maandalizi ya mwisho kabla ya AFCON, itakayopigwa kuanzia Desemba 21 nchini Morocco




