Mbappe aushukia uongozi PSG

FOWADI Kylian Mbappe ameunyooshea kidole uongozi wa Paris Saint-Germain kutokana na klabu hiyo kuishia njiani mara kwa mara katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Miamba hiyo ya Ligue 1 iliondolewa hatua ya 16 bora katika michuano hiyo msimu uliopita baada ya kushindwa kufua dafu mbele ya Bayern Munich katika mikondo miwili, Mbappe akikosa mkondo wa pili kwa sababu ya majeraha lakini alicheza PSG ilipopoteza kwa goli 1-0 nyumbani uwanja wa Princes.
Hatma ya Mbappe imekuwa ikitawala vichwa vya habari katika wiki za hivi karibuni baada ya kufahamika kuwa hakusudii kusaini mkataba mpya PSG akiwa amebakiza mwaka mmoja tu katika mkataba wa sasa.
Tovuti ya michezo, 90min inasema iwapo fowadi huyo mwenye umri wa miaka 24 hatasaini mkataba mpya au kuuzwa kipindi hiki cha dirisha la usajili, ataondoka PSG kwa uhamisho huru, jambo ambalo ni kero kwa Rais wa klabu Nasser Al-Khelaifi.
Al-Khelaifi amemwambia wakala wa Mbappe na mama mzazi wa mshambuliaji huyo Fayza Lamari kuhusu ni ya PSG kumuuza majira haya ya joto ili kupokea ada ya uhamisho, kitu ambacho mchezaji mwenyewe anaonekana hana nia kukifanya kwani anataka kusubiri.
Lakini kushindwa kwa PSG wakati uliopita ni mada kuu ya mahojiano ya hivi karibuni ya Mbappe akiwa katika majukumu ya kimataifa na kikosi cha Ufaransa na hakusita kuwashoonshea kidole walioko madarakani PSG kutokana mambo kuendelea kuwa kinyume.
“Tulifanya tulichoweza. Unapaswa kuzungumza na watu wanaounda timu, wanaopanga kikosi, wanaojenga klabu hii. Mimi, ninajaribu tu kufanya kazi yangu vizuri iwezekanavyo,”amesema Mbappe.
Mbappe ameongeza kuwa : “Nilifunga takriban mabao arobaini kwa klabu. Nilikuwa mchezaji bora, mfungaji bora kwa mwaka wa tano mfululizo kwenye Ligue 1. Katika Ligi ya Mabingwa, kwa bahati mbaya, niliumia kabla ya mechi ya mkondo wa kwanza na, tuliporejea, hatukuwa na nguvu. Lakini katika hatua ya makundi nilikuwa mchezaji aliyeamua matokeo. Ndio maana sio suala kubwa kuhusu mimi lakini zaidi kwa uongozi.”
Habari zinadai tayari Real Madrid imekubali kumsajili Mbappe bure msimu ujao ingawa uhamisho huo unaotarajiwa bado haujakamilishwa.