Mbappe aibeba tena Madrid, yaifumua Bilbao

MADRID: MSHAMBULIAJI wa Real Madrid Kylian Mbappé meisaidia klabu hiyo kukomesha mfululizo wa matokeo mabaya baada ya kucheza mechi tatu za ligi bila ushindi baada ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi ya goli wakati klabu yake ilipoichapa Athletic Bilbao mabao 3-0 usiku wa Jumatano.
Eduardo Camavinga pia aliifungia Madrid, ambayo sasa imerejea kuwa pointi moja tu nyuma ya Barcelona baada ya ushindi wao wa 3-1 dhidi ya Atletico Madrid siku ya Jumanne.
Mechi za raundi ya 19 za LaLiga zilisogezwa mbele kutokana na Madrid, Barcelona, Athletic Club na Atletico Madrid kuwa na majukumu ya kucheza Super Cup ya Hispania mwezi Januari nchini Saudi Arabia.
Madrid ilikuwa imetoka kutoshana nguvu na Girona, Elche na Rayo Vallecano katika mechi zake tatu zilizopita za ligi, huku ushindi huu ukiwa wa pili tu katika mechi zao sita za karibuni kwenye mashindano yote.

“Ilikuwa muhimu, baada ya sare tatu ugenini. Timu ilianza mchezo kwa umakini, nguvu na kasi tangu dakika ya kwanza. Huenda hii ikawa mechi yetu bora zaidi msimu huu.” kocha wa Madrid Xabi Alonso amesema.
Mbappé aliendeleza ubora wake wa kufumania nyavu, na kufanya idadi yake kufikia mabao saba katika mechi zake tatu zilizopita. Alifunga dhidi ya Girona, kisha mabao manne dhidi ya Olympiakos katika ushindi wa 4-3 wa Ligi ya Mabingwa.
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa sasa ana jumla ya mabao 30 katika mechi 24 za msimu huu kwa klabu na taifa, na anaongoza chati za ufungaji kwenye LaLiga akiwa na mabao 16, pamoja na Ligi ya Mabingwa akiwa na mabao tisa.




