Mayanga, Mashujaa FC yametimia

DAR ES SALAAM: Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kati ya uongozi wa Mashujaa FC na Kocha Salum Mayanga, hatimaye kila kitu kimekamilika kwa asilimia kubwa, na kinachosubiriwa sasa ni utambulisho rasmi wa kocha huyo mpya.
Mayanga, kwa sasa anakinoa kikosi cha Mbeya City, anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa kocha mkuu wa Mashujaa FC. Atachukua nafasi ya Mohammed Abdallah “Bares,” aliyeng’olewa kutokana na mwenendo mbaya wa timu katika mashindano mbalimbali.
Taarifa kutoka ndani ya klabu zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamekamilika kwa asilimia 99. Hivi sasa, kinachosubiriwa ni Mayanga kuwasili Kigoma kwa ajili ya kumalizana na viongozi wa Mashujaa FC na kuanza rasmi majukumu yake mapya.
“Ni kweli tulikuwa na mazungumzo na Mayanga, na tumefikia sehemu nzuri, tunatarajia kumtambulisha rasmi na kumpa jukumu la kukiongoza kikosi chetu katika michezo iliyosalia ya mzunguko wa pili, pamoja na mechi ya Kombe la Shirikisho la CRDB,” amesema mmoja wa viongozi wa Mashujaa FC, ambaye hakutaka kutajwa jina lake.