Matola: Hakuna mechi nyepesi Ligi Kuu

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema kikosi chake kinauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, akisisitiza kuwa hakuna mechi rahisi katika ligi hiyo.
Simba watacheza mchezo wa Ligi Kuu kesho dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo saa moja jioni.
Akizungumza kuelekea katika mchezo huo, Matola alisema maandalizi yamekuwa thabiti na dhamira ya timu ni moja tu kurejea kwenye ushindi.
“Tunauchukulia mchezo huu kwa umuhimu mkubwa kwa sababu kwenye ligi hakuna timu nyepesi. Pamoja na ugumu huo, tumejipanga na kufanya maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kushinda na kupata pointi tatu kwenye mchezo wa kesho,” alisema Matola.
Beki wa Simba David Kameta alisema timu imeimarika vizuri na wamefanya kazi ya kurekebisha makosa ya mchezo uliopita, huku wakija na mbinu mpya zitakazowapa nafasi ya kutafuta matokeo chanya.
“Wachezaji tumefanya maandalizi ya kutosha na katika mechi ya kesho tutakuja na mbinu nyingine tofauti na mchezo uliopita ili kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema.
Simba inatafuta kurejea kwenye mwenendo mzuri baada ya kuanza vibaya kwenye majukumu ya kimataifa.





