Mao: Azam FC lazima tuweke alama Afrika

JUBA:MCHEZAJI mkongwe wa Azam FC, Himid Mao, amesema kikosi hicho kimedhamiria kupambana kwa nguvu zote ili kuacha alama kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup).
Akizungumza akiwa kambini Juba, Sudan, Mao ambaye amewahi kucheza klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Misri, alisema wachezaji wamejipanga kupambana “kufa au kupona” kuhakikisha Azam inafanikisha malengo iliyojiwekea ya kufanya vizuri katika mashindano hayo makubwa.
“Kila mchezaji anatambua umuhimu wa mashindano haya. Tunataka kuandika historia mpya kwa Azam FC, kwa hiyo tumejipanga kupambana kuanzia mchezo wa kwanza,” alisema Mao.
Azam FC ipo nchini Sudan kwa ajili ya mchezo wake dhidi ya Al Merreikh, wapinzani ambao wamewahi kukutana nao miaka ya nyuma. Hata hivyo, Mao alisema safari hii wanataka matokeo tofauti yatakayowapa nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Licha ya kushiriki mara kadhaa michuano ya kimataifa, Azam FC haijawahi kufika hatua za juu kama ilivyofanikiwa kufanya vigogo Simba na Yanga. Hali hiyo imeifanya timu hiyo kuwa na shauku ya kufanya makubwa na kuandika historia mpya katika mashindano ya mwaka huu.