Kwingineko

Man City yakwama kwa Monaco.

MONACO: KLABU ya AS Monaco ya Ligue 1 imeambulia sare ya 2-2 nyumbani dhidi ya Manchester City kwa penalti ya dakika za jioni iliyofungwa na Eric Dier baada ya wageni hao kushindwa kutumia vyema ubora wao katika raundi ya pili ya mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya usiku wa kuamkia leo.

Dier alifunga penalti hiyo katika dakika ya 90 na kufuta uongozi wa mabao mawili ya Erling Haaland ya kipindi cha kwanza, baada ya awali Jordan Teze kuisawazishia timu hiyo ya Ufaransa. Penalti hiyo iliinyima Man City ushindi wa kwanza ugenini katika kipindi cha miezi 12.

Kikosi cha Pep Guardiola, ambacho kilifungua kampeni kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Napoli, sasa kina pointi nne kwenye msimamo wa ligi hiyo kikiwa nafasi ya nane huku Monaco wakiwa nafasi ya 30 na pointi moja baada ya kupoteza 4-1 dhidi Club Brugge katika raundi ya kwanza.

“Sidhani kama tulicheza vizuri vya kutosha. Hatustahili kushinda tukiwa hivi. Tunahitaji nguvu zaidi. Tulihitaji kufanya zaidi ya yale tuliyofanya katika kipindi cha kwanza. Tuliwatawala zaidi na wao wakafanya hivyo kipindi cha pili. Haitoshi.” – Haaland alisema baada ya mchezo huo

Manchester City itasafiri kuwafuata Villarreal katika raundi inayofuata ya ligi hiyo Oktoba 21 na Monaco itawakaribisha Tottenham Hotspur siku inayofuata.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button