Man City, Doku kinakaribia kueleweka

KLABU ya Manchester City inatarajiwa kunasa saini ya winga machachari Jeremy Doku baada ya kukubaliana na timu ya Rennes ada ya pauni milioni 55 sawa na shilingi bilioni 170.2.
Doku mwenye umri wa miaka 21 huenda akawemo kwenye kikosi cha kocha Pep Guardiola kitakachoikabili Sheffield United Agosti 27 katika mechi ya Ligi Kuu England kwenye uwanja wa Bramall Lane.
Mchezaji huyo alikuwa kwenye rada ya City tangu katikati ya msimu uliopita lakini nia ya kumsajili imeongezeka kufuatia kuondoka kusikotarajiwa mwezi uliopita kwa Riyad Mahrez kwenda Al-Ahli ya Saudi Arabia.
Usajili wa Doku unatarajiwa kuongeza nguvu kwa Guardiola ambaye mwisho wa wiki iliyopita amekiri kwamba kikosi chake kinahitaji wapiganaji zaidi.
Doku alifunga mabao sita akiwa Rennes Ligi Kuu Ufaransa, Ligue 1 msimu uliopita na anajulikana kwa kupelekesha theluthi moja ya mwisho ya timu pinzani.