Majaliwa kufungua Shimiwi leo
WAKATI michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inatarajiwa kufunguliwa rasmi leo, baadhi ya timu za mihimili ya serikali ikiwamo Ofisi ya Rais Ikulu na Ofi si ya Bunge zimeshindwa kufurukuta kwenye michezo yake ya kuvuta kamba.
Timu hizo zimeshindwa baada ya wanaume kuvutwa na wapinzani wao katika uwanja wa shule ya sekondari ya Usagara.

Michuano hiyo iliyoanza Oktoba 2, kwenye viwanja mbalimbali jijini Tanga, itafunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Katika michezo iliyofanyika ya miamba, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wamevutwa na Idara ya Mahakama kwa 2-0, wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) waliwavuta Ofisi ya Bunge kwa 2-0.
Timu nyingine zilizoshinda kwa mivuto 2-0 kwa wanaume ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) waliwavuta Wizara ya Katiba na Sheria, nao Wizara ya Maliasili waliwavuta ndugu zao Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Wizara ya Elimu waliwavuta Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi).
Kwa upande wa wanawake timu zilizoshinda kwa mivuto 2-0 ni Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) waliwavuta Ofisi ya Bunge huku RAS Simiyu wakiwavuta Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi.
Nayo Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara waliwavuta RAS Singida huku Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) waliwavuta Bohari ya Dawa.
Katika mchezo wa netiboli kwenye Uwanja wa Bandari, Timu ya Ofisi ya Rais Ikulu imewafunga RAS Dar es Salaam kwa mabao 60-8, nayo Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imewachapa RAS Mbeya mabao 19-7, huku Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepata ushindi wa mabao 40 baada ya timu ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kutokufika uwanjani.
Katika mchezo wa soka kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari Popatlal, Wizara ya Afya waliwapiga bila huruma RAS Dar es Salaam kwa mabao 4-0, wakati Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) waliwafunga RAS Lindi kwa mabao 4-0.




