Mahakama yatupilia mbali pingamizi la Jux,
Kesi ya umiliki wa nyimbo kusikilizwa Februari 26, 2026

DAR ES SALAAM: MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imetupilia mbali pingamizi la msanii Juma Musa maarufu kama Jux, katika kesi ya madai inayomkabili, na kuamuru shauri hilo kuendelea kusikilizwa Februari 26, 2026.
Kesi hiyo imefunguliwa na mtayarishaji na msanii Shabani Abdalla Shaban maarufu kama Keizer Pie, anayodai kuwa ni mwandishi mwenza wa asilimia 50 wa baadhi ya nyimbo maarufu za Jux.
Nyimbo zinazotajwa kwenye shauri hilo ni pamoja na Uzuri Wako, Nitasubiri, Wivu, Nikuite Nani, Sisikii na Your Mine, ambazo Keizer Pie anasema alishiriki kuzitunga.
Kupitia kesi hiyo, anaiomba mahakama itambue rasmi mchango wake kama mtunzi mwenza na apewe haki zake, ikiwemo malipo ya mirabaha yatokanayo na nyimbo hizo.
Kwa upande wake, Jux aliwasilisha pingamizi la kisheria akidai kuwa kesi hiyo imepitwa na muda wa kufunguliwa kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, mahakama imekataa hoja hiyo na kueleza kuwa shauri lina msingi wa kuendelea kusikilizwa, hivyo pande zote zitaendelea na mchakato wa kisheria.
Shauri hilo sasa limetajwa tena Februari 26, 2026, ambapo litatajwa na kuendelea kusikilizwa rasmi.




