Mabedi: Tunajua kuna presha, tutapambana

DAR ES SALAAM: KOCHA Msaidizi wa Yanga Patrick Mabedi, amesema wachezaji wake wanatambua ukubwa wa presha waliyonayo kuelekea mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers ya Malawi, lakini wamejiandaa kupambana kuhakikisha wanapata ushindi na kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Akizungumzia mchezo huo Dar es Salaam jana Mabedi alisema kwenye mpira kila mchezo una presha, na wao wanaishi kwenye hiyo presha.
“Tunajua kuna presha kubwa hasa kwa mashabiki wetu, lakini jambo muhimu kwenye mchezo wa kesho ni kufanya vizuri na kusonga mbele ili kuondoa hiyo presha. Wachezaji wote wamejiandaa vizuri na wako tayari kuipambania nembo ya klabu yetu,” alisema Mabedi.
Yanga inashuka dimbani kesho ikiwa nyuma kwa bao 1–0, baada ya kupoteza mchezo wa kwanza uliochezwa mjini Lilongwe, Malawi wiki iliyopita.
Ili kusonga mbele, Wananchi wanahitaji ushindi wa angalau mabao mawili nyumbani bila kuruhusu goli.
Mabedi alisema kuwa kikosi chake kitalazimika kushambulia tangu dakika ya kwanza ili kufuta pengo la bao moja lililopatikana katika mchezo wa kwanza.
“Kesho tunatakiwa kushambulia tu, hatutakiwi kukaa nyuma. Tayari wapinzani wetu wako mbele kwa goli moja na tunatakiwa kuhakikisha tunashinda mchezo wa kesho ili tusonge mbele – huo ndio ukweli na hakuna njia nyingine,” alisema Mabedi.




