Lizer Classic: Acheni kuchanganya mambo

DAR ES SALAAM: Muandaaji maarufu wa muziki nchini, Lizer Classic, amesema kuwa uwekezaji unaofanywa kwa wasanii katika tasnia ya muziki unalenga kazi zao za muziki pekee na si maisha yao binafsi.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Lizer Classic ameandika ujumbe akieleza kuwa wasanii wengi husahau mipaka iliyopo kati ya uwekezaji wa muziki na maisha binafsi.
“Wasanii wengi huwa wanasahau kuwa mwekezaji anapowekeza kwake anawekeza kwenye muziki wake tu na sio maisha yake binafsi,” ameandika.
Amefafanua kuwa mara nyingi wawekezaji wanaowekeza kwa wasanii hulenga kukuza kazi zao za muziki na si kuwajibika kugharamia maisha yao ya kila siku.
Hata hivyo, amebainisha kuwa endapo mwekezaji atachangia au kusaidia hata katika maisha binafsi ya msanii, hatua hiyo hutokana na upendo au uamuzi wake binafsi na si sehemu ya makubaliano ya uwekezaji wa muziki.
Kauli ya Lizer Classic imeibua mjadala miongoni mwa wadau wa tasnia ya muziki, huku baadhi wakijiuliza kama ujumbe huo unamlenga msanii au tukio fulani ndani ya tasnia hiyo.
Hata hivyo, muandaaji huyo hakutaja jina la msanii au mtu yeyote anayehusishwa moja kwa moja na ujumbe huo.




